Mwanamuziki wa Uganda, Jose Chameleone ambaye jina lake kamili ni Joseph Mayanja, ameomba radhi kwa kumbusu mwanamuziki na ndugu yake wa kiume Weasle Manizo kwenye mdomo wakati alipokuwa jukwaani kwenye onesho la muziki wake siku ya Ijumaa katika mji mkuu, Kampala.
Hii si mara ya kwanza kwa ndugu hao kupigana mabusu jukwaani, lakini hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja nchini, huku kukitolewa wito wa kuwakamata wanaoendeleza tabia hiyo ya mapenzi ya jinsia moja.
Busu la Jose Chameleone na kaka yake mwanamuziki Weasel lilimfanya mhubiri mashuhuri nchini humo kutoa malalamiko kwa polisi dhidi ya wawili hao.
"Ninajua nimewakwaza marafiki zangu na mashabiki zangu wengi waliudhika. Ninaomba radhi sana. Ilikuwa ni msisimko wa jukwaani na kiukweli najuta," mwanamuziki huyo alisema kwenye video yake ya Twitter.
Mlezi wa jumuiya ya Wanamuziki wa Uganda alisema amewasiliana na Mchungaji Martin Ssempa kwa nia ya kuondoa malalamiko hayo dhidi ya Jose Chameleone.
Aidha, Bunge la Uganda siku ya Jumanne lilimpa mbunge wa upinzani ruhusa ya kuwasilisha mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja, ambao alisema ulikusudiwa kushughulikia uandikishaji, upandishaji vyeo na ufadhili wa shughuli zinazohusiana na mahusiano ya watu wa jinsia moja.
Mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria nchini Uganda, ambapo wanaweza kuadhibiwa hadi kifungo cha maisha jela kwa kufanya "makosa yasiyo ya asili".