“NIMETUMA kitabu changu cha hadithi ya ‘Kubali Tuyamalize’ unisaidie kuandika ‘script’ ya filamu yangu ijayo, sijui kama umekipata… nahitaji kutengeneza filamu… Nataka stori hii iwe filamu na Mwenyezi Mungu akiniweka hai, InshaAllah, itakuwa moja ya filamu nzuri sana!”
Hayo ni maneno ya mwisho kabisa ambayo mzee Amri Mbwana Makata Bawji aliniambia kwenye simu, nikiwa Jijini Dar es Salaam na yeye akiwa nyumbani kwake Barabara ya 9, Jijini Tanga, wiki chache tu kabla mauti hayajamfika.
Katika mazungumzo yetu, tuliweza pia kukumbushana mengi kuhusu namna gani tuna deni la kuandika riwaya hasa baada ya kuhamasika kutokana na Tamasha la Mjue Mtunzi lililoandaliwa na Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi) na lililowakutanisha watunzi na wasomaji wao.
Hata hivyo, katika mazungumzo yetu kwenye simu niliweza kubaini kuwa Mzee Bawji hakuwa buheri wa afya, alikuwa na maumivu. Lakini pamoja na maumivu aliyokuwa nayo, mzee huyo hakuonesha kukata tamaa, walau aliweza kuzungumzia kitu tofauti na maumivu yake.
Kwa kawaida, binadamu anapokabiliwa na maumivu makali, hicho ndicho kipimo halisi cha kumfahamu yeye ni mtu wa aina gani na anafikiria nini.
Mzee Bawji aliweza kuzungumzia filamu na riwaya huku akiwa na maumivu na amebakiza wiki chache tu za kuishi hapa duniani, jambo linalothibitisha kwamba utunzi na sanaa kwa ujumla vilikuwa ndani ya damu yake.
Kwa kweli tasnia ya uandishi wa riwaya, sanaa na wapenda burudani kwa ujumla tumepata pigo kwa msiba huu uliotushtua wengi, wafuatiliaji na wasio wafuatiliaji wa riwaya na filamu, kutokana na kifo cha mzee wetu, Amri Bawji.
Mzee Amri Bawji amefariki dunia usiku wa Februari 21, 2021 wakati akipokea matibabu kwenye Hospitali ya Bombo jijini Tanga, alipolazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
Binafsi nilimfahamu Mzee Bawji miaka ya mwanzoni mwa tisini kupitia hadithi zake katika jarida la SANI. Historia yake inaonesha kuwa alianza kuchapisha riwaya zake kupitia majarida ya Sani mwaka 1993.
Baadaye alisajili jarida la AMBHA na kuendeleza tungo zake, huku kipaji kingine cha uandishi wa mashairi kikionekana. Majarida hayo yalikuwa maarufu sana kipindi hicho, kabla ya baadaye kuanza kutoa riwaya zake kwenye gazeti la Kiu ya Jibu.
Tangu nikiwa mdogo nilipenda sana kusoma riwaya, kila nilipopata uwezo wa kusoma nilipenda kusoma hadithi za watunzi mahiri wakiwemo Eddie Ganzel, Shaban Robert, Faraji Katalambula, John Rutayisingwa, Agolo Anduru, Juma Mkabarah na Hammie Rajab.
Wakongwe wengine walionivutia ni Euphrase Kezilahabi, Ben R. Mtobwa, Amri Bawji, Elvis Musiba, Jackson Kalindimya, Lucy Nyasulu na wengineo wa zama hizo. Watunzi hawa ndiyo walionifanya nivutiwe kupenda kuandika.
Nakumbuka nilikutana na Mzee Amri Bawji kwa mara ya kwanza mwaka 2001 aliponitafuta kwa ajili ya kujadili kuhusu muswada wake wa filamu ya “Augua”, kwani alikuwa katika maandalizi ya kutengeneza filamu hiyo, ambayo kwake ilikuwa ya pili, baada ya kupata udhamini toka Mfuko wa Utamaduni.
Kabla ya mjadala wetu aliniomba nitazame kwanza sinema yake ya kwanza ambayo alikuwa ameshaitoa ya “A Love Story – Tanganyika na Unguja”.
Siku hiyo tulikutana katika eneo la Kinondoni, nyumbani kwa msanii Nina. Hatukuwa peke yetu, walikuwepo pia watu wengine watatu.
Penye wengi pana mengi, katika kuichambua filamu ya ‘A Love Srory – Tanganyika na Unguja’ mengi yaliongewa, ya kufurahisha na mengine ya kukera lakini niliweza kutambua kuwa Mzee Amri Bawji, kama mwandishi mkongwe, alikuwa anajua jinsi ya kumchukulia mtu hata kama ameongea jambo la kuudhi.
Mara kwa mara hakusita kupokea maoni na ushauri, na hata unapomkosea, Bawji alikuwa hakasiriki au kuonesha chuki kama walivyo waandishi wengine. Sana sana alijaribu kukuelekeza kwa upole!
Huo ni upande mmoja tu wa Mzee Bawji, kama mwandishi mahiri wa riwaya na filamu. Lakini ukweli ni kwamba mzee huyu wa Kidigo kutoka Tanga, alijaaliwa vipaji vingi mno.
Alikuwa mtunzi wa hadithi, mwandishi wa miswada ya filamu na makala za televisheni, mwanafilosofia, mtunzi wa mashairi na kadhalika.
Hadi mauti yanamkuta mzee Amri Bawji alikuwa ameshaandika zaidi ya riwaya 12, miswada mbalimbali ya filamu iliyozidi kumng’arisha katika fani ya uandishi, mashairi na kutoa vitabu viwili vya riwaya; ‘Kubali Tuyamalize’ na ‘Muafaka’.
Kuingia kwa Mzee Bawji katika tasnia ya uandishi wa riwaya kupitia jarida la SANI kulitokana na kifo cha mdogo wake ambaye pia alikuwa mmiliki wa jarida hilo, Said Mbwana Bawji, aliyeliasisi jarida hilo akiwa na rafiki yake, Nico Ye Mbajo. Sani ni kifupi au herufu za mwanzo za majina Saifi na Nico.
Hata hivyo, Said Bawji kabla ya kifo chake mwaka 1993, alikuwa ameshatoa vitabu viwili vya riwaya vya “Usiku wa Balaa” na “Pumbazo la Moyo” vilivyompa umaarufu mkubwa, na hivyo ujio wa Amri Bawji katika kuendeleza kazi ya mdogo wake kulifanikiwa kuliimarisha na kuling’arisha jarida la SANI.
Katika safari yangu ya uandishi na utunzi, Amri Bawji alikuwa mmoja wa waandishi wakongwe walionitia moyo, nani yeye aliyenishauri kuzingatia zaidi msuko wa matukio niandikapo hadithi.
Msuko wa matukio unahitaji sana creativity (ubunifu) na inspiration (msukumo).
Ni Amri Bawji aliyeniambia kuwa unapotunga stori yoyote inayohitaji kuyasuka vizuri matukio katika hadithi yako unahitaji sana kufanya meditation (taamuli au tafakuri ya kina) na utafiti wa kile unachokiandikia.
Katika utunzi, inafika wakati mtu unakwama na kujikuta ukiwa huna kitu cha kuandika. Mtunzi mzuri akishaona hana kitu cha kuandika ataacha kuandika kwa muda na kuzama katika tafakuri ya kina ili apate kitu bora cha kuendelezea hadithi yake badala ya kukurupuka tu ilimradi amalize.
Nimelishuhudia jambo hili toka kwa watunzi wa riwaya wengi wa zama zetu, wengi wanakosa uvumilivu na hawana muda wa kutafakari kwa kina au kufanya utafiti na matokeo yake huishia kuandika hadithi zinazopwaya au hunakiri hadithi za wengine na kubadilisha mtazamo kidogo tu, na hivyo kukosa msuko mzuri wa matukio.
Kwa kweli msuko mzuri wa matukio katika hadithi ndiyo utamfanya msomaji hadithi apate hamu ya kuendelea mbele zaidi ili kujua nini kitatokea.
Kifo cha Amri Bawji kinaongeza idadi ya watunzi mahiri wa riwaya hapa nchini walioaga dunia, watunzi ambao binafsi nakiri kuwa walikuwa hazina bora kwa taifa hili na nimejifunza mengi kutoka kwao.
Watunzi wengine mahiri waliotangulia ni pamoja na Shaban Robert, Eddie Ganzel, Agolo Anduru, Ben R. Mtobwa, Elvis Musiba, Kassim Chande, Rajabu Mbega, John Rutayisingwa, Faraji Katalambula, Hammie Rajab, Jackson Kalindimya, Euphrase Kezilahabi na wengine ambao siwakumbuki.
Mzee Amri Bawji alizaliwa mwaka 1947 huko Ngamiani Mkoa wa Tanga, mkoa ambao nauhusudu sana kwani umekwishatoa magwiji wa burudani katika nyanja zote za sanaa, burudani na michezo hapa nchini.
Mzee Bawji amekuwa kielelezo cha mafanikio makubwa ya tasnia ya uandishi wa riwaya nchini, kutokana na kazi zake nyingi kupata umaarufu mkubwa na hivyo kuchagiza sana kukua na kuimarika kwa tasnia ya uandishi wa riwaya nchini.
Kama ambavyo imekuwa ikisemwa, Mzee Bawji alifahamika pia kama mtaalamu wa kutunga misemo na methali zilizotumika katika kuyang’arisha majarida mbalimbali, mfano “Wapambe nuksi”; “Ukupigao ndiyo ukufunzao”; “Mchele mmoja mapishi mbalimbali”; “Mfa maji haishi kutapatapa”; na misemo mingine mingi iliyompa umaarufu mkubwa.
Pia mkongwe huyu wa riwaya hakuwa nyuma kwenye suala zima la utengenezaji wa filamu, kazi zake zilizotamba na zinazokumbukwa zaidi ni pamoja na filamu ya “A Love Story – Tanganyika na Unguja” iliyotoka mwaka 1998, ikitokana na riwaya yenye jina hilo hilo ya mwaka 1995.
Filamu hii ilikuwa moja ya sinema zilizotamba kwenye majumba mbalimbali ya sinema kipindi hicho, sambamba na filamu za kutoka nje hususan za Bollywood (India).
Nakumbuka iliwahi kutamba katika majumba ya sinema kama Majestic Cinema (Tanga), Empire Cinema (Dar es Salaam), Metropole Cinema (Arusha), Liberty Cinema (Mwanza) n.k.
Kuoneshwa kwa kazi hii kwenye majumba ya filamu kulizidi kumpa umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi.
Ningeweza kuandika mengi kumhusu gwiji huyu wa riwaya na filamu lakini nafasi haitoshi, naamini wapo waandishi wengine wanaomfahamu na kuyajua mengi, tutarajie pia kusikia lolote kutoka kwao ili tuzidi kujifunza mengi kutokana na maisha ya nguli huyu wa riwaya na filamu.
Amri Bawji ameondoka na bila shaka sote tutamfuata, lakini ametuachia hazina kubwa ya kazi zake ambazo daima zitadumu nasi na tabuia yake ya upole na kupenda kusikiliza. Ametufunza kuwa na mapenzi na watu, huruma, bashasha na ucheshi.
Mungu amrehemu Amri Bawji, na kazi zake ziendelee kudumu ili kizazi chetu na kizazi kijacho kizidi kufaidi zaidi matunda ya kazi zake.