Bodi ya Filamu nchini imesema mdahalo wa wasanii na wadau wa filamu nchini wa Aprili 29 utatoa elimu mahususi kwa wasanii wa filamu nchini kuanza kutumia fursa ya kuuza kazi zao kidijitali.
Huo utakuwa ni muendelezo wa mdahalo kama huo uliofanyika Mei mwaka jana na kuwashirikisha wadau mbalimbali zaidi ya 200 kutoka maeneo mbalimbali chini.
Katibu mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dk Kiagho Kilonzo amesema mitandao ya kijamii ni sehemu ya wasanii wa filamu kujitangaza, lakini wengi wao hawaitumii ipasavyo.
"Tumeandaa mdahalo kwa kushirikiana na SoshoNaMimi ili kutoa elimu kwa wasanii wa filamu njia bora ya kutumia teknolojia ya kidijitali kuuza kazi zao," amesema Dk Kilonzo.
Mwanzilishi wa SoshoNaMimi Saida Khalifan 'Shadee Weriss' amesema mdahalo huo utafanyika kwenye ukumbi wa CRDB, Dar es Salaam ukiwahusisha watoa mada wabobezi.
"Ni jukwaa la kuwapa elimu ya namna bora ya kuuza kazi zao mitandaoni na kutumia teknolojia kwa faida na kujitangaza, kutafuta masoko ya filamu katika mitandao," amesema Shadee na kuongeza.
"Sasa tunashirikiana na Bodi ya filamu kutoa elimu hii ambayo ni mahususi kwa wasanii wa filamu kupata elimu ya matumizi yenye tija kwenye mitandao ya kijamii.
Irene Ngao ambaye ni Afisa maendeleo ya Filamu wa bodi hiyo amesema ni wakati sasa wa wasanii wa filamu nchini kujikita kwenye masoko ya kidijitali.
"Dunia inatubadilisha, tunapaswa kutoka kwenye kuuza kazi zetu kawaida na kuuza kidijitali, bila shaka mdahalo wa Aprili 29 utakuwa ni fursa kwa wasanii wengi.