Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bobi Wine, Sugu, Jaguar wanavyochangamsha

13775 Pic+bobi+wine TanzaniaWeb

Sat, 25 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wimbi la wasanii Afrika Mashariki kutikisa kwenye siasa linazidi kuongezeka. Wanasiasa waliotoka kwenye sanaa hususan muziki wamekuwa na ufuasi mkubwa baada ya kujiingiza katika siasa.

Bobi Wine wa Uganda, Profesa Jay, Sugu na Jaguar wa Kenya ni miongoni mwa wanamuziki wanaotingisha anga la siasa Afrika Mashariki.

Kwa wiki nzima Afrika Mashariki ilikuwa ikifuatilia siasa za Uganda. Bobi Wine aliyekuwa na umri wa miaka mitatu wakati Rais Yoweri Museveni anachukua madaraka, amegeuka kuwa nguzo ya siasa za upinzani nchini Uganda. Tukio la kukamatwa kwa Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyaluganyi na kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi na baadaye ya kiraia limevuta hisia za watu wengi Afrika Mashariki. Maandamano ya mitaani na yale ya mitandaoni yanathibitisha nguvu ya sanaa na siasa hasa katika nchi za Afrika Mashariki.

Wafuasi wa mwanasiasa huyo huru, waliibua mjadala mtandaoni na baadhi wakimhoji Rais Yoweri Museveni ambaye alishindwa kujizuia kujibu na kutoa tamko kueleza namna ambavyo suala la kushikiliwa kwa Bobi Wine linaweza kushughulikiwa.

Raia wa Uganda wanaoishi Kenya na Uingereza walifanya maandamano wakitaka aachiwe, mawakili 24 walijitolea kumtetea na katika mtandao mjadala ulikuwa mkali na wananchi hawakusita kumuhoji Rais wao moja kwa moja kupitia mtandao wa Twitter.

Katika hatua nyingine siasa za Afrika Mashariki zilihamia nchini ambapo mwanzoni mwa mwaka huu jina la Mbunge wa Mbeya, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu lilipotikisa anga kufuatia hukumu ya kifungo cha miezi mitano kwa madai ya kumkashifu Rais.

Sugu, anayetamba na wimbo wake mpya alioupa jina la namba ‘219’ alivuta ufuasi mkubwa kutokana na hukumu hiyo ambayo aliitumikia mpaka Mei 10, mwaka huu.

Mbali na kuvutia siasa kutokana na kesi yake, Sugu ndiye mbunge pekee nchini aliyeshinda kwa kura nyingi 108,566 mwaka 2015.

Mbunge wa Mikumi, Profesa Jay ambaye amewahi kutamba na kibao cha ‘Zali la Mentali’ naye anazipamba siasa za Afrika Mashariki akiwa mbunge wa upinzani baada ya kumwangusha mpinzani wake Jonas Nkya wa (CCM). Charles Njagua maarufu kwa Jaguar alikuwa msanii wa kwanza nchini Kenya kupenya katika siasa na kufanikiwa kuwa Mbunge. Aliibuka mshindi wa Jimbo la Starehe kwa asilimia 53 ya kura zote, huku akifuatiwa na Steve Ndwiga aliyepata asilimia 31 na Boniface Mwangi aliyeambulia asilimia 13.

Jaguar ambaye wimbo wake wa ‘Kigeugeu’ ulishika kasi ameendelea kuwa kielelezo cha sanaa katika siasa nchini humo hasa katika harakati za kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana wenzake.

Akizungumzia siasa na sanaa, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema miongoni mwa sifa za mwanasiasa ni kuwa maarufu kulingana na mambo aliyokuwa akifanya huko nyuma au anayofanya wakati anaowania nafasi husika.

Alisema bila umaarufu mwanasiasa hawezi kujulikana na itakuwa ngumu kujenga ushawishi kwa wananchi, hivyo kwa wasanii inakuwa rahisi kwa sababu tayari wana wafuasi waliokuwa wakifuatilia sanaa yao na wanapohama huhama nao.

“Sanaa ndiyo eneo pekee unaloweza kutengeneza ushawishi na kuwa na wafuasi wengi kwa muda mfupi, hivyo wanaofanya vizuri kwenye sanaa ni rahisi kuwa na ushawishi kwenye siasa, ”alisema na kuongeza:

“Ingawa msanii akiingia kwenye siasa akitokea chama tawala anaweza asifanye vizuri zaidi kwa sababu atakuwa anasifia, labda awe na ajenda tofauti sana kama alivyokuwa marehemu Amina Chifupa ambaye aliwagusa wananchi moja kwa moja alipoamua kupambana kuhusu dawa za kulevya, ”alisema.

Dk Mbunda alifafanua kuwa, “Ukiingia kwa tiketi ya upinzani una nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwa sababu utakuwa ni mkosoaji mkubwa na mtetezi wa wananchi hususani ukilenga suala la demokrasia ambalo kwa nchi za Afrika bado lina shida na utatuzi wa kero mbalimbali ikiwamo huduma za afya, maji na elimu.

Chanzo: mwananchi.co.tz