Mwimbaji tajiri kutoka Guinea, Moussa Sandiana Kaba almaarufu Grand P anaonekana kusonga mbele na maisha yake miezi kadhaa baada ya kutengana na mwanasoshalaiti maarufu wa Ivory Coast, Eudoxie Yao.
Mahusiano ya Grand P na kipusa huyo mwenye umbo la kustaajabisha kweli yalifika kikomo mapema mwaka jana kwa njia isiyoeleweka baada ya wawili hao kuchumbiana kwa takriban miaka mitatu.
Katika siku za hivi majuzi,mwanamuziki huyo bilionea kutoka Guinea amekuwa akionekana na mwanadada mwingine mwenye asili ya Kiasia, Yubai Zhang, ambaye anaonekana wazi kuwa mpenzi wake mpya.
Wawili hao wamekuwa wakisafiri katika nchi tofauti pamoja na kujivinjari pamoja katika sehemu mbalimbali nzuri.
"Niko pamoja na mpenzi wangu Grand P, safari yangu nyingine inakuja hivi karibuni," Bi Zhang alisema siku kadhaa zilizopita kwenye video iliyomuonyesha akifurahia muda na mwimbaji huyo mbilikimo.
Siku ya Alhamisi, Grand P alithibitisha mapenzi yake na mrembo huyo wa Kiasia na kuweka wazi kuwa hakuna nafasi ya watu wenye wivu maishani mwao.
"Yubai Zhang wangu, hakuna nafasi kwa watu wenye wivu," alisema chini ya picha zake na Zhang alizochapisha Facebook.
Haya yanajiri miezi kadhaa tu baada ya bilionea huyo kujigamba kuhusu uhusiano wake usioweza kuvunjika na Eudoxie.
Mapema mwaka jana, Grand P aliweka wazi kuwa ataishi kumpenda mrembo huyo aliyebarikiwa na makalio makubwa kweli katika siku zote za maisha yake.
"Wewe na mimi ni kwa maisha. Shukran" Grand P alimwandikia Bi Yao.
Mwanamuziki huyo alisisitiza kuwa ndoa yake na mwanasoshalaiti huyo kutoka Ivory Coast ni imara na ya kudumu.
"Wanandoa wa milele, upendo wetu ni dira ya wenye wivu" Grand P alisema.
Mwanamuziki huyo mwenye maumbile ya kipekee aliendelea kumsherehekea mpenzi huyo wake wa zamani kwa jumbe tamu za mapenzi hadi mahusiano yao yalipogonga ukuta wakati usiothibitishwa mwaka jana.