Waziri wa Nishati, January Makamba, Balozi wa Mfuko wa maendeleo ya Ulaya (EU), Manfredo Fanti na feter Malika wa mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji ya Uwekezaji (UNCDF), wamekabidhi hundi zenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.2 kwa makampuni 16 yanayojishughulisha na usambazaji wa Nishati safi ya Kupikia.
Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dar ers Salaam, kufuatia Wajasiriamali hao kutuma maombi ya Ufadhili kwa UNCDF yaliyopokelewa kuanzia Septemba 2022 hadi February 1, 2023, kupitia mpango wa Cookfund unaolenga matumizi ya teknolojia ya Nishati safi ya kupikia.
Katika hafla hiyo, Waziri Makamba, amesema, “Tumeanzisha mfuko huu wa Nishati safi ya Kupikia kwa ajili ya Wajasiriamali wanaojishughulisha na usambazaji ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi wapate huduma hii, Na hawa ni wale waliokua wanakwama kusambaza nishati safi sababu za Mitaji kwenye mikoa mbalimbali Nchini.”
Waziri Makamba ameongeza kuwa, “Wanufaika hawa wako 16 na fedha hizi sio mikopo ni Ruzuku, Niwaombe waliopata pesa hizi wakazifanyie kazi husika ili tusionekane matapeli, Huu ni msaada unaotolewa kwa Nchi kutoka Umoja wa Ulaya, Msaada huu hauendi kwa Serikali unakuja kwa Wananchi moja kwa moja, Nyie mnaopata leo mkiharibu watu wanaofuata hawatopewa. Zimetengwa Bilioni 23 na leo tumetoa Bilioni 3.2 tu hivyo tuwe waaminifu.”
Aidha, amesema bado wanaendelea kukamilisha maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha taasisi za Kiserikali zenye watu zaidi ya 300 kuachana na nishati chafu ya kupikia, na waanze matumizi ya Nishati safi ya kupikia ambapo Mwishoni mwa mwezi Februari 2023 wanatarajia kutangaza rasimu ya Dira ya mpango huo.