Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Berlinale: Lupita Nyong'o aweka historia katika tamasha la filamu la Ujerumani

Berlinale: Lupita Nyong'o Aweka Historia Katika Tamasha La Filamu La Ujerumani Berlinale: Lupita Nyong'o aweka historia katika tamasha la filamu la Ujerumani

Fri, 16 Feb 2024 Chanzo: Bbc

Mwigizaji wa Kenya Lupita Nyong'o ameweka historia kwa kuchukua wadhifa wa kiongozi wa kwanza mweusi wa jumba la majaji la Tamasha la Kimataifa la Filamu la Berlin.

Tukio la kila mwaka la maonyesho ya filamu, pia linajulikana kama Berlinale, ni mojawapo ya matamasha matano makubwa ya filamu duniani.

Jopo hilo la Tamasha halijakuwa na mkuu mweusi katika historia yake ya miaka 74, waandaaji waliambia shirika la habari la AFP mwaka jana.

Nyong'o ataongoza jopo hilo katika kuchagua filamu zitakazoshinda katika orodha mbili kuu za Golden na Silver Bears.

Matamasha matano makuu ya filamu za kimataifa ni - Berlin, Cannes, Venice, Sundance na Toronto - mara nyingi yamekabiliwa na ukosoaji kwa kukosa uwakilishi wa watu wa rangi tofauti.

Tamasha kubwa zaidi na la pili kati ya haya, tamasha la Cannes, lilikuwa na rais wake wa kwanza mweusi 2020, wakati muelekezaji wa filamu nchini Marekani Spike Lee alipochaguliwa.

Katika ufunguzi wa hafla hiyo katika mji mkuu wa Ujerumani siku ya Alhamisi, Nyong'o alisema "ana heshima kubwa" kuchukua nafasi hiyo.

Aliongeza kuwa utofauti wa jopo hilo utaboresha mchakato wake wa kuamua juu ya filamu zitakazoshinda tuzo.

"Huo ndio uzuri wa kuwaleta watu wa asili tofauti - tunajibu kwa vitu tofauti," mwigizaji huyo, ambaye alishinda tuzo ya Oscar kupitia filamu ya 12 Years A Slave mnamo 2014.

"Tuna uzoefu na maoni mengi ya ulimwengu na itakuwa ya kuvutia. Pengine pia itakuwa bora zaidi."

Wakati Berlinale alipomtangaza Nyong'o kama rais wa jopo Disemba mwaka jana, wakurugenzi wa tamasha hilo, Mariƫtte Rissenbeek na Carlo Chatrian, walisema Nyong'o alichaguliwa kwa sababu "anajumuisha kile tunachopenda katika filamu", kupitia uigizaji wake wa aina mbalimbali na uwezo wa kuhudumia watazamaji tofauti.

Tukio hilo litaendelea hadi Februari 25, wakati jopo litatangaza filamu zilizoshinda katika orodha kuu.

Washiriki watatu wa Kiafrika ni miongoni mwa 20 wanaoshindania tuzo ya juu, na wote wanasimulia hadithi kutoka bara Afrika.

Miongoni mwao ni pamoja na Black Tea, iliyoandikwa na mkurugenzi wa Mali mzaliwa wa Mauritania, Abderrahmane Sissako, Who do I belong to ilioandikiwa na muelekezaji wa Tunisia-Canada Meryam Joobeur na makala ya Dahomey ya mtengenezaji filamu Mfaransa-Senegal Mati Diop.

Chanzo: Bbc