Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bendi zetu zinaelekea wapi?

49518 Pic+bendi

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika wiki mbili zilizopita nimepata bahati ya kuzunguka miji kadhaa hapa nchini. Lengo la safari ilikuwa za kujifunza mambo yanayoendelea katika tasnia ya muziki.

Katika kila mji niliopita nilijitahidi kutafuta taarifa za bendi zilizopo na zilizowahi kuwepo na kukutana na wanamuziki na wapenzi wa muziki.

Kuna miji ambako shughuli za muziki ziko katika hali nzuri sana. Nimekuta katika mji mmoja kumetengenezwa kituo cha wasanii ambacho kimeshaanza kufundisha muziki kwa watu wa aina mbalimbali, watoto na watu wazima na tena waalimu wakifanya kazi hiyo kwa kujitolea.

Nilipata bahati ya kualikwa na mdau mmoja ambaye ana chuo kinachotoa stadi mbalimbali za maisha kwa vijana, yeye akaniambia ana nia ya kuanzisha elimu ya taaluma ya muziki chuoni kwake, hata madarasa ya somo hilo alikuwa amekwisha andaa. Ilikuwa faraja kubwa sana kupata nafasi kutembezwa chuo hicho.

Pia, nilikutana na vijana wengi waliokuwa wanafanya juhudi binafsi za kujiendeleza katika aina mbalimbali za muziki, ilikuwa inasikitisha kuona hawana mtu wa kuwapa muongozo sahihi, lakini hakika kuna mengi yanafanyika katika muziki huko ‘mikoani’, lakini kutokana na kukosekana waandishi wa kuandika habari hizo, kazi nzuri zinaendelea kimya kimya bila kutangazwa.

Lakini kwa niliyojifunza katika safari hizi nimeona nijiulize tena kuhusu mada ambayo imekuwa inaendelea katika vijiwe mbalimbali hasa vya muziki wa dansi, mada hiyo inahusu hali ya muziki wa bendi nchini, na safari yake huko mbele.

Katika miji yote niliyopita nimekuta kuna bendi, nyingine zenye vyombo duni nyingine zenye vifaa vizuri sana, lakini kuna mambo ambayo yanafanana sana, kwanza kuna utamaduni wa bendi hizi kupiga muziki kwenye kumbi za baa bila kiingilio. Jambo la pili ni bendi kuishi kwa kupiga nyimbo za bendi za zamani.

Jambo la tatu ni bendi hizi kupiga nyimbo zinazofanana, hivyo basi nyimbo ambazo hutazikosa ni kama vile Rangi ya chungwa ya Nyanyembe Jazz, Georgina wa Safari Trippers, Kalubandika ya Maquis, Masafa Marefu wa Tancut Almasi na nyinginezo. Tofauti ya bendi hizi inakuwa ubora wa upigaji.

Jambo jingine la kufanana ni kukuta ile hali ya bendi hizi kutokuwa na mpango wowote wa kujitangaza, unakuta bendi haijulikani hata palepale katika miji ambayo bendi ipo. Katika hali hii naona itakuwa vigumu sana kwa muziki wa dansi kupata maendeleo.

Kwa kawaida kujifunza historia husaidia kujua mazuri na mabaya yaliyotendeka zamani na hivyo kuwa na mwanga wa namna ya kwenda mbele.

Bendi kufanyia mazoezi na kuzipiga nyimbo za zamani ni namna ya kujua historia ya muziki wa Tanzania na ingekuwa busara sana kwa kutumia ujuzi huo, bendi zingejitengenezea tungo zao ambazo zingetegemewa kuwa bora kuliko nyimbo hizo za zamani ambazo bendi zimeng’ang’ania kuendelea kuzipiga.

Katika kufuatilia nimegundua bendi hizi nyingi hazifanyi mazoezi ya uhakika, hata hizo nyimbo za zamani zinapigwa kwa uzoefu tu, hivyo kutokuwa na ubora kama ilivyokuwa asili ya nyimbo hizi.

Katika miaka yote niliyokuwa kwenye bendi mbalimbali, jambo moja lilikuwa wazi mazoezi yalikuwa kitu muhimu sana, bendi ilipokuwa inataka nyimbo mpya au mwanamuziki kujiendeleza katika chombo anachopiga au kujiendeleza kama ni muimbaji, mazoezi ilikuwa ni lazima, hivyo kundi lisilokuwa na mazoezi hakika haliwezi kukua.

Jambo jingine lililonikosesha raha sana ni ukosefu wa nidhamu katika kazi. Kwa mfano siku moja niliingia katika baa fulani, nikakuta vyombo vya muziki na nikaambiwa kuwa baadaye siku ile kungekuwa na dansi la kukata na shoka kuanzia saa mbili usiku.

Saa mbili usiku nilifika kwenye baa ile nikamkuta DJ akiporomosha muziki kutoka kwenye CD zake, wanamuziki wa bendi walikuwa bado hawajafika, wahudumu wakanihakikishia kuwa lazima kutakuwa na dansi.

Mwanamuziki wa kwanza aliwasili saa tatu na nusu, na hatimaye kundi zima lilianza muziki saa nne na robo, haikuchukua muda mrefu kugundua kuwa wanamuziki walikuwa na tabia nyingine mbaya, walikuwa wakihangaika kuomba bia tena bila aibu kwa kutumia vipaza sauti.

Kifupi muziki ulichelewa kuanza na ulipoanza ulikuwa ni kero ya wanamuziki kutaja majina ya wafadhili ili wanunuliwe vinywaji. Kwa kuangalia haya machache unaona kabisa baadhi ya mambo yanayosababisha muziki wa dansi kupungua thamani.

Wanamuziki wengine wamekuwa wakitupia lawama vyombo vya utangazaji hasa redio na luninga kuwa havirushi nyimbo zao, wakati huohuo hawajarekodi nyimbo mpya.

Wanamuziki wengine wamekuwa wakishangaa kwa nini wanadharauliwa lakini tabia zao ni wazi ni mbaya kiasi cha kuwa vigumu kuheshimiwa. Kwa kweli kuna haja ya wanamuziki wa muziki wa dansi kujitathmini upya katika kazi zao ikiwa kuna nia ya kurudisha thamani ya muziki wa dansi tena.



Chanzo: mwananchi.co.tz