Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Belle 9, Ben Pol wanavyokiwasha Hip Hop Bongo

Belle Pic Data Belle 9, Ben Pol wanavyokiwasha Hip Hop Bongo

Mon, 9 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Hakuna ubishi Belle 9 na Ben Pol ni miongoni mwa wanamuziki wachache ndani ya Bongo Fleva wanaofanya vizuri katika upande wa miondoko ya RnB na tayari wametengeneza himaya ya utawala wao upande huo.

Wamekuwa wakifanya muziki unaopendwa na wengi na hata wasanii wenzao na kutokana na ubora wa kazi zao wamejikuta wakifanya kolabo nyingi sana na wasanii wakubwa wa Hip Hop jambo linaloashiria kupendwa pia kwamuziki huo. Hebu tazama;.

Weusi

Wasanii kutoka kundi la Weusi, Bonta, Joh Makini na Nikki wa Pili ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe sasa wamewahi kufanya kazi na wakali hawa wa RnB.

Mwaka 2012 Nikki wa Pili alimshirikisha Belle 9 katika wimbo wake uitwao Hatuendani chini ya Prodyuza Mona Gangstar, licha ya ubora wa wimbo huu Nikki hakuona sababu ya kufanyia video yake.

Kisha Bonta pamoja na Nikki wa Pili wakamshirikisha Ben Pol katika wimbo wao unaoitwa Usirudi Jela uliyopikwa na Prodyuza Nahreel, Nikki akafanya tena wimbo na Ben unaoitwa Sitaki Kazi ambao ulifanya vizuri sana.

Naye Joh Makini akamshirikisha Ben Pol katika wimbo wake Simwachii Mungu huku Ben akimshirikisha katika ngoma yake iitwayo Unanichora. Naye Belle 9 akamshirikisha Joh Makini katika wimbo wake Vitamin Music ambao ulifanya vizuri na ndio ukawa mwanzo wa kufungua lebo yake, Vitamin Music Group (VMG).

Tamaduni Muzik

Rapa Nikki Mbishi ndiye msanii pekee wa Tamaduni Muzik aliyefanya kolabo na wote wawili kwa vipindi tofauti akiwa chini ya lebo ya M Lab ambapo Ben Pol alikuwepo pia.

Nikki alimshirikisha Belle 9 kwenye wimbo uitwao Si Lazima uliopikwa na Prodyuza Den Texas wa M Lab Studio, pia katika wimbo huu yupo One The Incredible na Marehemu Godzilla ambaye hakuwa sehemu ya Tamaduni Muzik.

Kwa upande wa Ben Pol, alishirikishwa na Nikki Mbishi katika wimbo Play Boy ambao ulifanya vizuri na kumtoa Nikki kimuziki pia alishiriki katika wimbo mwingine Pata Raha ambao One The Incredible na Stereo walishirikishwa, nyimbo hizi mbili zilitayarishwa na Duke Tachez.

Sugu na Afande Sele

Kwa sasa hawa wote ni wasanii wakongwe walioamua kutimkia kwenye siasa na licha ya ukongwe wao wameweza kutambua uwezo vijana wapya katika muziki wa RnB.

Utakumbuka Sugu alimshirikisha Belle 9 kwenye wimbo uitwao Ukinipa Nafasi ambao yupo na Mwana FA, ngoma hii ilipikwa na Marehemu Prodyuza Pancho Latino.

Kisha Belle 9 akapewa shavu tena na Afande Sele msanii mwenzake kutoka Morogoro aliyeshinda shindano la Mkali wa Rhymes mwaka 2004, ni katika wimbo unaokwenda kwa jina la Dini Tumeletewa.

JCB na Nyandu Tozzy

Hawa ni wasanii wa Hip Hop ambao muziki wao ni ule tunaoweza kusema ni mgumu, JCB akiwakilisha kundi lake la Watengwa, huku Nyandu Tozzy akiwakilisha B.O.B.

JCB alimshirikisha Ben Pol katika wimbo wake I donĂ­t Care ambao ulitengenezwa na Maprodyuza wawili, Defxtro (DX) wa Noizmaker na J Ryder wa Tongwe Records.

Nandu Tozzy alimpa shavu Belle 9 katika wimbo wake uitwao Kwa Mashabiki ambao walikuwepo pia Young Killer na Young Dee, wimbo huu ulitayarishwa na Prodyuza Mona Gangstar.

Fid Q na Young Killer

Hawa ni wachanaji wanaofanya vizuri kutoka jijini Mwanza, uzuri ni wote wawili wametambua uwezo wa Belle 9 na Ben Pol na kuwa nafasi katika ngoma zao.

Ben Pol ameshashirikishwa na Fid Q katika wimbo uitwao Bendera ya Chuma uliyotayarishwa na Director Nisher, ni miongoni mwa nyimbo alizozitumbuiza Fid Q ndani ya Coke Studio Africa.

Kwenye wimbo wa Young Killer uitwao 13 aliwashirikisha Fid Q na Belle 9 ambaye aliimba kiitikio cha wimbo huo huku pia watatu hawa wakitoa wimbo mwingine uitwao Hatuna Kesi.

Kama hiyo haitoshi Belle 9 ndiye aliupaisha wimbo wa Young Killer, Dear Gambe ambao ndio ulimtambulisha na kumtoa kimuziki na kushinda tuzo ya Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) mwaka 2014 kama Msanii Bora Chipukizi.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz