Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashungwa: TaSUBa ongezeni ubunifu

76400d9873e9f3a86d3c6a1d55f310a5 Bashungwa: TaSUBa ongezeni ubunifu

Tue, 22 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (pichani) ameitaka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), kuongeza kasi na ubunifu wa kitaaluma katika kuutangaza utamaduni wa Tanzania kimataifa.

Aidha ametaka taasisi hiyo iendelee kuwazalisha wahitimu wenye weledi na ujuzi mkubwa katika sekta ya utalii, sanaa na utamaduni ili wachangie kukuza zaidi uchumi wa nchi kupitia sera ya viwanda.

Bashungwa aliyasema hayo jana alipotembelea taasisi hiyo, kujionea shughuli za kitaaluma zinazofanyika chuoni hapo, ikiwa ni sehemu ya ziara zake katika taasisi zilizo chini ya wizara yake tangu ateuliwe kuwa waziri.

Katika ziara hiyo aliambatana na Naibu Waziri, Abdallah Ulega na Katibu Mkuu, Dk Hassan Abbasi. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea taasisi hiyo, Bashungwa alieleza kuridhishwa na namna vijana wanavyoandaliwa kitaaluma katika kuingia katika ajira na kujiajiri katika soko la utamaduni, sanaa na utalii. Alitaka kasi zaidi ya kutangaza nchi kimataifa.

“Hii ni sehemu ya ziara zetu kutembelea taasisi zilizo chini yetu. Hapa tumeona programu mbalimbali kikubwa ni TaSUBa kuongeza kasi kutangaza sanaa na utamaduni wetu kimataifa ili utumike kukuza uchumi kupitia sera ya viwanda,” alisema Bashungwa.

Alisema wao wataendelea kushirikiana na taasisi hiyo, kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanachagiza maendeleo ya sanaa na utamaduni wa Tanzania na kutumika kukuza uchumi wa nchi na vijana, ambao wengi wako katika sekta hizo ikiwa ni pamoja na kuchochea utalii zaidi nchini. Bashungwa alisema lipo soko la Afrika Mashariki (EAC) na la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Alisema lengo la serikali ni kuona bidhaa zinazozalishwa kutokana na utamaduni na sanaa, zinatoa kipato kikubwa kwa vijana, wahusika na taifa. Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Herbert Makoye, alisema taasisi hiyo imepokea maelekezo yote ya kuongeza ubunifu kwa jicho la kiuchumi ndani na nje ya nchi ili kuitangaza nchi.

Dk Makoye alisema mwakani wataanza programu mpya zinazogusa sanaa za asili, ili kupata wanafunzi wengi kutoka nje ya nchi. Alisema wameongeza udahili kutoka wanafunzi 308 mwaka jana hadi 651 mwaka huu.

Chanzo: habarileo.co.tz