Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Basata yafafanua makosa matano yaliyowapeleka kifungoni Diamond, Rayvanny

32517 Bastapic Diamond na Rayvanny

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Juzi Baraza la Sanaa (Basata), lilitangaza kuwafungia kwa muda usiojulikana wasanii Diamond Platnumz na Rayvanny likidai kufikia uamuzi huo baada ya wasanii hao kuonyesha dharau kwa mamlaka zinazosimamia shughuli za sanaa nchini, kwa kufanya vitendo vinavyokiuka maadili.

Mbali na kuwafungia wanamuziki hao, Basata imetangaza kukifuta kibali cha Tamasha la Wasafi Festival linaloendelea nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Onesmo Kayanda amefafanua makosa mbalimbali waliyofanya wasanii hao mpaka kufikia hatua ya kuwapa adhabu hiyo.

Alisema Diamond na Rayvanny walifanya makosa kwa kuutoa wimbo Mwanza bila kufuata taratibu ambazo zinawaelekeza kupeleka mashairi katika baraza hilo kabla ya kurekodi.

Aliongeza kuwa kosa lingine ni kuuruhusu wimbo huo uendelee kutazamwa katika mtandao wa Youtube hata baada ya kupigwa marufuku.

“Kosa lingine walifanya wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Wasafi mkoani Mtwara ambako Diamond alitamka matusi makubwa jukwaani. Wengi wameiona video ile akifanya hivyo. Sisi kama walezi tulimuonya,” alisema Kayanda.

Katika kupalia moto, Kayanda alisema Kampuni ya Wasafi haikupewa kibali cha tamasha hilo mkoani Mwanza kwa kuwa katika maombi haikuorodheshwa. “Kama walezi pia hatukuona busara kumzuia tukiamini litakapomalizika tutazungumza naye, lakini cha kustaajabisha huko akaimba wimbo ambao umepigwa marufuku.”

Pia, alisema msanii Giggy Money aliimba wimbo Nampa Papa katika tamasha hilo mkoani Morogoro wakati wimbo huo umepigwa marufuku kuimbwa au kupigwa mahali popote.

Mwana FA awafungulia milango

Baada ya kufungiwa kutofanya maonyesho ndani na nje ya nchi, wasanii Diamond na Rayvanny wameambiwa wanaweza kukata rufaa juu ya maamuzi hayo kwa bodi ya Basata.

Akizungumza na Mwananchi, Hamis Mwinjuma ’Mwana FA’, ambaye ni mjumbe wa bodi hiyo anasema bado wana nafasi ya kukata rufaa kama uamuzi huo hawajaridhika nao.

Mwana FA ambaye pia ni msanii wa muziki wa kizazi kipya, ameweka wazi kuwa, bodi haihusuki na kuwafungia wasanii hao kama inavyohisiwa, isipokuwa ni kazi za watendaji wa baraza hilo.

“Sisi katika hili la kufungia wasanii huwa hatuhusiki nalo katika majukumu yetu, bali ni la kiutendaji zaidi kwa baraza hilo.

“Kama msanii ikifika mahali akaona hajatendewa haki, anaruhusiwa kukata rufaa kwa bodi kueleza kwa nini anaona adhabu aliyopewa hastahili, tukiipitia tukiridhika na maelezo yake tunaweza kuja na majibu,” alifafanua.

Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa uwanja huo, Mwana FA alisema mpaka jana alikuwa hajapata taarifa ya wasanii hao kupeleka barua ya rufaa.

Wajumbe wengine wa Basata ni Dk Saudh Mwakaje ambaye ni Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwigizaji, Single Mtambalike, Asha Mshana ambaye ni mhadhiri msaidizi Idara ya Sanaa, Habari, Ubunifu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na Dk Emmanuel Ishengoma ambaye pia ni mhadhiri wa Udom.



Chanzo: mwananchi.co.tz