Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Basata wafunguka utata wa ukaguzi nyimbo za wasanii

Basata Pic Data.png Basata wafunguka utata wa ukaguzi nyimbo za wasanii

Wed, 5 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limewaondoa hofu wasanii na kueleza kuwa utaratibu wa kukagua nyimbo kabla ya kuchezwa kwenye redio na kuonyeshwa kwenye luninga, unalenga kuzipangia madaraja kulingana na mashairi na sio kuzifungia kama watu walivyoitafsiri.

Akizungumza na Mwanaspoti Online jana Jumanne Mei 4, 2021 alisema wameamua kufanya hivyo kama moja ya njia ya kulinda maadili na kuhakikisha kazi hizo zinaangaliwa au kusikilizwa kutegemeana na rika la watu na kuhakikisha zinazingatia maadili, mila na desturi.

Mniko alisema wakati kwa sasa kukiwa na manung’uniko ya kutekelezwa kwa kanuni hiyo, ukweli ni kwamba sheria hiyo ya mwaka 2018 kifungu cha 1 hadi cha 6,  ipo ambayo imeweka bayana nini msanii anapaswa kufanya katika kazi yake kabla hajaiwasilisha kwa walaji na wanachofanya kama Basata ni katika kuwakumbusha wasanii na vyombo vya habari kuhusu kanuni hizo.

 “Hii sheria sio ngeni katika kuitekeleza tumeanza nayo tangu mwaka 2018, lakini watu wanaiona kama ni ngeni jambo ambalo sio kweli  tunachokifanya ni katika kuwakumbusha wasanii wanachotakiwa kufanya ,” amesema Katibu huyo.

Alipoulizwa kwa nini msisitizo huo unakuwa sasa na sio huko nyuma, Mniko alisema kitu chochote kikishatungiwa sheria na kutengenezewa  kanuni, ukiona kunalegalega katika utekelezaji wake mnakaa kama menejimenti kukazia kwa kuwa tayari kanuni zipo.

Hata hivyo aliwaondoa wasiwasi wasanii kuhusu uharaka katika kukagua kazi zao na kueleza kuwa wamejipanga na wana watu wa kutosha ambapo nyimbo moja kukaguliwa haizidi hata dakika tano.

“Huenda wasanii wakawa na wasaiwasi kama kazi hii tunaweza kuitekeleza kwa wakati ukizingatia wasanii ni wengi na nyimbo mpya zinatoka kila siku, naomba niwaondoe shaka katika hili, kwani mpaka unapata majibu ndani ya muda mfupi.

“Pia katika ukaguzi huo tunatarajia kutumia njia mbalimbali ikiwemo  kutoa namba ya WhatsApp ambapo msanii hatalazimika kufika ofisini kwake na badala yake ataituma na kutumiwa majibu kupitia mtandao huo,” amesema Mniko

Kwa upande wa vyombo vya habari ikiwemo redio na luninga, aliomba ushirikiano ambapo amesema wasanii wanaopeleka nyimbo zao lazima ziambatane na barua ya Basata inayoeleza kuwa wimbo huo unakubaliwa kuruka na kwa muda gani.

Wakati kuhusu wanaorusha kupitia mitandao, Katibu huyo alisema huko watakutana na rungu la Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), mamlaka ambayo pia wanafanya nayo kazi kwa karibu katika kusimamia kazi za Sanaa.

Hata hivyo katika shughuli hiyo ya ukaguzi, Mniko amesema ni nadra kutokea wimbo ukakataliwa, zaidi wengi wanatakiwa wakazirekebishe.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz