Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baraka Magufuli aibukia Chato

1377d1a7045bf33d2a8cd2d377e6068e.jpeg Baraka Magufuli aibukia Chato

Fri, 26 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MSANII wa vichekesha, Baraka Mwakipesile ‘Baraka Magufuli’ amepata nafasi ya kuonesha kipaji chake cha kuiga sauti ya Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli katika shughuli ya kuaga mwili wa kiongozi huyo iliyofanyika jana Chato.

Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka huu kutokana na maradhi ya moyo na anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwake wilayani Chato.

Msanii huyo alikuwa akiigiza sauti ya kiongozi huyo tangu akiwa hai katika matukio mbalimbali na kujizolea umaarufu mkubwa na kupachikwa jina la Baraka Magufuli.

Baraka alizungumza kwa sauti inayofanana kwa kiasi kikubwa na kiongozi huyo ambapo ungeweza kudhani alikuwepo eneo hilo akizungumza.

Msanii huyo alizungumza machache kwa sauti ya msisitizo ya Rais Magufuli huku akiiga mapozi na vitendo alivyokuwa akionesha akizungumza wakati wa uhai wake. “Ametuachia alama katika taifa letu, lakini hili limekuwa ni fundisho kwa viongozi wa sasa kwamba nchi hii inatakiwa kuongozwa kwa namna gani.”

“Mungu wetu alimleta Magufuli kwasababu maalumu na amemuondoa kwasababu maalum, ndugu zangu ameiacha nchi ikiwa na amani, umoja na mshikamano kwelikweli,” alisema msanii huyo kwa sauti ya Rais Magufuli.

Alisema Magufuli ameiacha Tanzania yenye mwanga wa maendeleo, yenye uchumi wa kati, yenye vituo vingi vya afya na yenye umeme kwenye vijiji vingi.

“Wito kwa viongozi mlioko hapa, leo tunaye Rais mama Samia Suluhu, ndugu zangu Watanzania tushikamane kwelikweli, tumuunge mkono Rais wetu huyu na tumuombe Mungu ayaendeleze yaliyoachwa.”

“Mimi nisiwe muongeaji sana, nimekuja kumsindikiza baba yangu, niwape pole familia na viongozi wote, kwa kweli nimeumia sana,” alisema msanii huyo kwa sauti ya Magufuli.

Chanzo: www.habarileo.co.tz