Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Banana Zorro Adai subira ndiyo imemfanya adumu

9823 Babana+picTZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwaka 2007 ulikuwa mzuri kwa msanii Banana Zorro na hii ni baada ya kupokewa vizuri kwa albamu yake ya Mama.

Albamu hiyo ilikuwa imesheheni nyimbo mbalimbali ikiwemo Mama wenyewe uliobeba jina la albamu, Niko Radhi, Wasiwasi, Bado Kidogo, Mapenzi Gani na nyingine nyinginezo.

Wakati anatoa albamu hiyo ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kufanya kazi nje ya bendi yake ya Inafrica iliyokuwa imesheheni wasanii mahiri akiwemo Bob Rudala na Bizman.

Baadaye aliachia vibao vingine ikiwemo Zoba, Nzela na kile alichoshirikishwa na msanii mwenzake Afsa Kazinja kilichokwenda kwa jina la ‘Pressure’ kilichozidi kumuweka vizuri katika soko la muziki.

Pia katika harakati zake hizo za muziki, Banana aliwahi kushiriki shindano la kusaka vipaji la Cocacola Idol, lililowaibua wasanii wengine kama Langa (marehemu), Shaa na Whitney ambao sasa hivi wanafanya vizuri katika soko la muziki.

Pamoja na kuwa mwanamuziki wa muda mrefu huku akiwaacha wengine walioanza nao wakiishia njiani, Banana ameendelea kukimbizana na soko hilo hadi leo huku zaidi akijikita kwenye kuimba muziki wa kutumia vyombo.

Muziki huo mara nyingi anasema anaupiga katika hoteli mbalimbali na bendi yake ya Banana ambayo pia ndio ilimuibua msanii Nandy anayekimbiza kwa sasa katika muziki wa Bongo Fleva.

Siri ya kudumu sokoni

Akizungumza na gazeti la Mwananchi katika mahojiano maalumu, Banana ambaye ana zaidi ya miaka 15 kwenye muziki, anasema moja ya sababu ya kuendelea kufanya kazi hiyo ni subira.

Msanii huyu ambaye ni baba wa watoto wawili, anasema kwa sasa anachokiona kwa wasanii ambao alikuwa katika ushindani nao kipindi wanaanza muziki wa Bongo Fleva, ni kutokukubali kushindwa na wale wanaochipukia.

“Kuna ile kujiona kwa nini huyu ‘anashaini’ wakati mimi nimemtangulia kwenye ‘gemu’ pasipokujua kwamba kutangulia sio kufika na ili kukabiliana na hiyo hali yakupasa kuwa mbunifu ili usiachwe.

“Mbaya zaidi wengine wamefikia hatua hadi ya kuwekeana bifu pasipo sababu wakati wangepaswa kuwa viongozi kwa wasanii chipukizi na kuwaonyesha njia ya wapi wapite ili kufikia mafanikio ambayo wameyapata,” anasema.

Hata hivyo kwa upande wa wasanii wanaovuma na kupotea kwa muda mfupi, anasema kikubwa kwao kinachowatatiza ni kutaka mafanikio ya harakaharaka bila ya kuyatolea jasho.

Katika hili anasema msanii utakuta kaanza leo, lakini kesho anataka awe na mafanikio kama aliyokuwa nayo msanii ambaye yupo kwenye gemu muda mrefu huku akiwa tayari kutumia hata njia zisizo halali ili kupata umaarufu wa haraka.

“Mfano siku hizi kuna hiki kitu kinaitwa ‘kiki’, ambacho wasanii wenye kutaka kupata umaarufu haraka wanafanya tukio ambalo litakuwa gumzo katika mitandao ya kijamii na mtaani kwa ujumla.

“Wakati wakiyafanya hayo hawakumbuki kwamba hata mashabiki wake wanajua kuchuja mabaya na mazuri, ambayo binafsi kiki nyingi kwangu huwa naziona za mambo mabaya ambayo yanakushushia heshima mbele ya jamii na hadhira yako.

“Kama wasanii wenzangu hawatabadilika watakuwa kila siku wanalalamika kuwa soko ni gumu wakati ugumu wanausababisha wao na wakumbuke kuijenga heshima ni kazi na unapoiharibu kuirudisha huwa ni shughuli pevu,” anasema Banana.

Kwa upande wake msanii huyu ambaye ni mtoto wa mwanamuziki maarufu Ally Zahir Zorro, anasema kati ya vitu ambavyo anaviepuka ni pamoja na masuala hayo ya kiki kwani mbali na kumuharibia katika familia, pia kuna uwezekano mashirika mbalimbali aliyoingia nayo mkataba kumtosa.

Anasema moja ya mambo ambayo mashirika na watangazaji mbalimbali wanapenda kuona kwa msanii ni pamoja na kujiheshimu.

Heshima hiyo, anasema amewaambukiza hadi wasanii wa bendi yake kuwataka siku zote waishi hivyo bila kujali majina makubwa waliyo nayo kwenye jamii na kuongeza kuwa ndicho chanzo cha bendi yake kudumu.

Siri nyingine kubwa anasema ni yeye kukulia na kulelewa katika mikono ya wanamuziki, kwani mbali ya baba yake kuwa mwanamuziki, pia bendi aliyokuwa akifanyia kazi akiwa na umri mdogo imechangia kumfanya hivyo alivyo ambapo anapiga kila aina ya chombo cha muziki.

Hivi karibuni msanii huyo anatarajia kuachia kibao chake cha Sitanii, ambacho ameahidi kitawaonyesha mashabiki namna gani alivyo mwanamuziki na si msanii.

Chanzo: mwananchi.co.tz