Dar es Salaam. Mmoja wa viongozi kutoka lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Hamisi Taletale amesema yupo tayari kujenga ukumbi wa starehe hata kesho kama Serikali ya Tanzania itamruhusu.
Tale ameyasema hayo leo Jumatatu Julai mosi, 2019 alipozungumza na Mwananchi ikiwa ni siku chache tangu aweke andiko kwenye ukurasa wake wa Instagram kuhusu athari za kutokuwa na ukumbi huo.
Katika maelezo yake, Taletale kwa jina maarufu la Babu Tale amesema kuna wakati wanahitaji kualika wasanii maarufu nchini lakini kutokana na kutokuwa na ukumbi mzuri wanashindwa.
“Kuna watu wengi walishaahidi ujenzi wa ukumbi, lakini naona hakuna vitendo ila mimi hata kesho Serikali kama itaniruhusu nitajenga kwani nina wadau wengi ambao wanaweza kushirikiana nami katika kulifanya hilo.”
“Inaniuma sana kama mdau wa burudani, ukiangalia wenzetu wa michezo ya mpira na mengine wana sehemu ya kujidai lakini sisi wa burudani tunaishia kufanya shoo kwenye maeneo yenye vumbi na kama mvua itanyesha huenda onyesho likaahirishwa,” anasema Babu Tale ambaye ni mmoja wa Meneja wanaomsimamia msanii maarufu Tanzania Diamond Platnumz.
Kwa upande wake, Katibu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Susan Mlawi alipotafutwa kulizungumzia hilo amesema, “Kama Serikali hatuwezi kufanya kazi na mtu kwa kuandika kwenye Instagram au kumwambia mtu mmoja.”
Pia Soma
- UDSM yabuni mashine ya kisasa ya kutotoreshea vifaranga
- Papa aiona amani mkutano wa Trump, Kim
- Waziri Ummy abainisha mambo matatu ya kutofautisha hospitali na vituo vya afya
- Takukuru wamdaka mzazi akitoa rushwa ili mtoto wake aliyefaulu asiendelee na masomo
“Badala yake anachopaswa kufanya Babu Tale ni kupeleka nyaraka za ombi hilo la ujenzi Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ambao hao ndio wana mamlaka ya kupitia andiko lake.”
Mlwi amesema, “Huko Basata watamuelekeza namna gani ukumbi huo unapaswa kujengwa, halafu wao watatufikishia sisi kwa ajili ya vibali na mambo mengine.”