Sakata la lebo ya WCB kudaiwa kuwanyonya wasanii wake huku lebo ikijineemesha bado halijatamatika, mmoja wa mameneja wa lebo hiyo amefunguka tena akidai kwamba wao kama WCB wanawekeza pesa nyingi kwa msanii hivyo ni halali kukata hicho kiasi kwani hiyo ni biashara hata wasanii wakubwa wa Marekani wanafanya.
Babu tale ameenda mbali zaidi na kusema WCB si ya kwanza kukata wasanii kwani hata malkia wa muziki duniani, Beyonce anakatwa asilimia 70 na lebo yake huku yeye akiambulia asilimia 30 pekee.
"Beyonce anachukua asilimia 30 kwenye mkataba wake na huyo ni Queen wa dunia kwenye muziki. Ukiona sisi (Wasafi) tunachukua hicho tunachokichukua ni tofauti, Wasafi wakikuchukua wakianza kuweka hela kwako.
“Yani tumeanza kuweka hela leo kesho unafanya shoo, hatuanzi kukukata zile pesa (zilizo tumika kuku-brand) ni unachukua cha kwako, Wasafi wanachukua cha kwao.
"Kinachochukuliwa na Wasafi hakihesabiwi kwenye kile ambacho kilitoka kwa ajili yako kwa ajili ya kuwekeza, hatujawahi kukata kabisa yani kitakapoanza kuingia hata kesho pesa yako iko palepale 40 yako 60 ya label wamewekeza ni biashara,'' amesema Babutale.