Dar es Salaam. Siku chache baada ya kutangaza kuokoka, msanii Godfrey Tumaini maarufu ‘Dudu Baya’ amesema watu watarajie kuona mabadiliko katika muziki wake.
Dudu Baya ameyasema leo Jumatatu Agosti 26, 2019 alipozungumza na Mwananchi ikiwa ni siku moja ipite tangu alipotangaza kuokoka akiwa katika Kanisa la Arise and Shine la mchungaji Boniface Mwamposa.
Amesema kutokana na kuamua kuoka maisha yake kwa sasa ikiwemo muziki utabadilika na kuwaambia mashabiki zake watarajie kumuona kwenye muziki wa Injili.
Kama vile haitoshi, amesema hata katika mashairi ya nyimbo zake za bongo fleva, hatakuwa akiweka maneno aliyoyaita machafu kama alivyokuwa akifanya huko nyuma.
“Nimeamua kubadili mfumo wangu wa maisha kuanzia ninavyoishi mtaani hadi kwenye kazi yangu ya muziki, hivyo mashabiki nawahakikishia kuanzia sasa nyimbo zangu hazitakuwa na maneno machafu kama ilivyozoeleka,” amesema
“Kwani nimeamua kutumia kipaji changu katika kutoa elimu zaidi na ninawashauri watu kumtumaini Mungu kwani yeye ndio kila kitu katika maisha yao,”.
Pia Soma
- Majeruhi mmoja ajali ya moto Morogoro afariki, vifo vyafikia 102
- Rais Magufuli awaita Ikulu watendaji kata wote
- Kesi inayomkabili Halima Mdee, Hakimu atoa nafasi ya mwisho
Jana Jumapili, Agosti 25, 2019 Dudu Baya alikwenda kanisani kwa Mwamposa Kawe jijini Dar es Salaam ambapo akimtambulisha mbele ya waumini, Mchungaji Mwaposa alisema msanii huyo alimfuata siku ya Jumamosi kanisani kwake na kuomba amuombee.
Mchungaji Mwamposa alisema alilazimika kufanya hivyo kwa kuwa watu kama Dudu wanahitaji neema ya msaada kwani wasiposaidiwa watakwenda kutafuta msaada kwa waganga wa kienyeji na kuongeza alipofika kwake alimuombea na sasa amekuwa kiumbe mpya.