Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baa za Didi's, Element, Jackies za Masaki zabomolewa

28899 BOMOA+PIC TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama ni miongoni mwa wanaopenda kwenda maeneo ya starehe Masaki jijini Dar es Salaam, kuanzia leo ukifika maeneo hayo hutaamini utakachokiona.

Baa maarufu zilizokuwepo Masaki kando ya barabara ya Haile Selassie mfano Eaters point, Didi’s, Jackie’s na Element zimebomolewa kufuatia agizo la Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), kutokana na kuwa ndani ya hifadhi ya barabara.

Meneja wa Tarura wilayani Kinondoni, Leopold Runji alisema kama wahusika hawataondoa wenyewe kama walivyokubaliana watawaondoa kwa nguvu.

“Tulikubaliana tangu Juni mwaka huu lakini wamedharau kuondoka au kubomoa, juzi (Ijumaa iliyopita) tumeweka alama ya X kuwakumbusha. Hatuna muda wa kuwapa, waondoe sasa na wasipofanya hivyo tutawaondoa kwa nguvu,” alisema Runji.

Mwananchi lilishuhudia baa za Jackies na Didi’s zikibomolewa na wahusika wenyewe huku Element ikiwa imefungwa na ubomoaji ukiendelea.

Kufuatia ubomoaji, maeneo hayo yamekuwa madogo kiasi kwamba hayawezi kuwa kama awali hata kama biashara itaendelea.

Meneja wa Jackie’s, Godwin Moshi alisema taarifa ya Tarura kuwataka wabomoe ilitolewa Ijumaa iliyopita ikiwataka kubomoa na kuondoka wenyewe mapema hadi kufikia kesho kwa waliojenga mita 50 ndani ya hifadhi ya barabara.

“Jackie’ s iko hapa miaka zaidi ya 20, hili lina athari kubwa kwetu kibiashara, inabidi biashara isimame ili kujenga upya,” alisema.

“Itatugharimu sana kutokana na hali ya uchumi wa sasa. Notisi imekuja ghafla bora hata ingekuja wiki tatu au mwezi kabla.”

Alisema eneo lililobaki ni dogo kwa biashara na hivyo itawalazimu kuandaa upya mpango wa biashara.

Katika ufafanuzi wake Runji alisema, “barabara za Masaki ni pana kuliko zote lakini hazina mifereji, maana yake nini? Lile eneo la pembeni mwa barabara lililoachwa wazi ndiyo linachukua nafasi ya miferej.”

“Wapo waliojenga mitaro kimsingi wanaziba mitaro na kupitisha maji ambayo hutuama barabarani na kuharibu barabara ya lami.”

Amesema kwenye kikao walichokaa na wananchi wa maeneo hayo na wenyeviti wao wa Serikali za mitaa walikuwapo.

Kuhusu wanaodai wamepewa vibali na manispaa ya kuendelea kufanya shughuli zao alisema, “Kikao walikaa na Tarura, sio manispaa. Tarura ndio inayoshughulika na barabara na manispaa wanajua kama wapo na wanafanya kazi yao bila kuingiliwa kwa sababu hawavunji sheria.”

“Hajawekewa X mtu aliye nje ya mipaka ya barabara, tumekuwa tukisema kila siku sasa ni utekelezaji, tunafufua mipaka yote ya barabara na kama umejenga hata ukuta na ukaona umeziba mtaa bora uondoe mwenyewe” alisisitiza.



Chanzo: mwananchi.co.tz