Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

'BOSI' RUGE KATUPA TALAKA TATU...

Thu, 28 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

'Bosi Ruge'. Aliitwa hivyo mpaka na watu baki siyo 'staff' wa Clouds tu. Wanamuziki, waigizaji, na watangazaji wa radio zingine walimuita 'Bosi Ruge'. Ilikuwa kama kuanza na neno Mheshimiwa kwa Wabunge na viongozi wa kisiasa. Mazingira haya yalitokana na namna yeye alivyowezesha watu wengi kwa miaka mingi.

Bosi Ruge ni mshikaji mmoja hivi 'simpo' kimwili, sauti na mavazi yake. Usingemdhania. Ukiisikia sauti yake utampuuza. Na aina ya mavazi yake siyo shawishi kiasi cha kumpa thamani kubwa. Lakini kwa kile kinachoendelea mjini hivi sasa utaelewa alikuwa mtu wa aina gani. Huyu ni mwamba wa biashara ya burudani Afrika Mashariki.

Baada ya mwendo mrefu sana. Kaachana na sisi rasmi bila kuregemea. Alifunga pingu za maisha na biashara ya burudani. Sasa katoa talaka tatu. Kila kitu alikigeuza kuwa burudani kabla ya kuwa mfereji wa kuingizia pesa. Anabaki kuwa miongoni mwa binadamu waliopunguza 'stress' za watu wengi sana nchini.

Kulikuwepo na radio na kulikuwa na Clouds ambayo ilikuwa zaidi ya radio. Kilikuwa kiwanda cha kuzalisha siyo tu vipaji bali akili mpya kwenye sekta ya burudani. Na jamaa ndiye aliyehusika zaidi kucheza mchezo wote. Na siku zote jamaa aliamini kwenye kipaji zaidi. Ni akili iliyotengeneza akili zingine.

Mwishoni mwa miaka ya tisini. Kuibuka kwa Clouds kulienda sambamba na ujio wa biashara kubwa ya burudani. Kama masihara vile, ubunifu mwingi na kujua jinsi ya kutumia vipaji vya watu kama Mzee Onyango, Mwita Maranya na wenzao. Kukafanya Clouds iwe juu ya radio zote. Ikawa biashara ndani ya biashara.

Wakati unafikiria Ruge ni mtu anayeibua wanamuziki wengi. Hutakosea. Ila kumbuka asilimia tisini ya watangazaji wa Clouds ni vipaji zaidi ya elimu. Jicho na akili ya Ruge ilimuibua Gardner G Habash na kuwa kioo cha watangazaji wengi hii leo. Ndivyo ilivyo lwa Masoud Kipanya na kina Gerald Hando. Achana na kina Diva hawa na wenzao kibao.

Kabla ya Fiesta kulikuwa na kitu kilichoitwa Summer Jam. Wanamuziki na wasanii wakapata jukwaa kubwa zaidi la kutangaza kazi zao na kujiongezea mashabiki zaidi ndani na nje ya nchi. Summer Jam ni tamasha la kwanza kuunganisha wasanii wa Afrika Mashariki. Na sasa ni Fiesta. Akili ya Ruge.

 

Alijenga mazingira ya pesa ya burudani ipite kwenye mbavu zake. Ikamate na kufuata kile anachotaka. Kusaga jicho lake lilikuwa kwenye namba za akaunti. Ruge akiwa 'master plan' wa namna ya kuendelea kutengeneza pesa zaidi. Mbali wazo la kuanzisha Clouds, kuwa na Ruge ilikuwa bahati kubwa zaidi kwa Kusaga.

 

Hakujua kuimba ila alifahamu nani anafaa kuimba. Hakuwa na muonekano wa utangazaji hata sauti yake haikufaa kwenye mawimbi ya radio. Lakini alijua na kusema ''I think utafaa kwenye Bambataa'". Ni baada ya kumsikiliza Gardner G Habash kwa mara ya kwanza akitaka shavu la utangazaji Clouds.

Kwenye mtiririko wa pesa hakuwa na adui. Akijua hii pesa alijishusha. Mafanikio ya Jide mpaka Nandy. Yeye anahusika. Ndivyo ilivyo kwa Chilla mpaka Diamond. Kuna mkono wake ndani ya mafanikio yao. Kwa hili hawawezi kukana hata muda huu akiwa hawezi hata kuchezesha kope. Walipitia kwake kuelekea Kaanani yao ya muziki.



Chanzo: mwananchi.co.tz