Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BINTI: Filamu ya viwango vingine

2ee3770633b142818449a92b41b33467 BINTI: Filamu ya viwango vingine

Sat, 10 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BINTI ni filamu iliyotumia mwaka mzima kuandaliwa huku kazi kubwa ikifanywa na wadau wa filamu akiwemo Seko Shamte anayemiliki Alkamist Media huku Angela Ruhinda na Alinda Ruhinda wakimiliki Kampuni ya Black Unicorn Studio.

Filamu hiyo imegusa changamoto za kimaisha ambazo wanawake wengi wanapitia iwe kwenye mahusiano, uchumi, afya na masuala mengie mbalimbali.

Washiriki wake wamefanikiwa kuuvaa uhusika hasa katika kuendana na kile kinachokusudiwa kufikishwa kwa jamii huku ujumbe mkubwa ukiwa ni kuwataka wanawake wanaopitia changamoto mbalimbali za kimaisha kutokata tamaa.

Filamu hiyo kwa asilimia kubwa imeakisi maisha ya mjini, ambapo Seko anasema kuwa imeshirikisha mazingira ya Mbezi, Temeke, Sinza, Masaki, Oysterbay, Upanga na Mikocheni yote ni maeneo ya Dar es Salaam.

Anasema ndani ya mwaka mmoja wa uigizwaji wake, filamu hiyo imeigiziwa maeneo hayo kwa nyakati tofauti tofauti usiku na mchana.

Imegusia sehemu kuu nne, ambazo ya kwanza inamuonesha Bertha Robert anayetumia jina la Sanaa Tumaini, mwanamke huyu alikuwa akijihusisha na ujasiriamali, ambapo pia alikuwa na mikopo mbalimbali.

Mikopo hiyo ilimkosesha amani kiasi cha kuchukua uamuzi wa kuchukua pete ya ndoa ya mama yake na kuiuza ili apate fedha za kulipia madeni.

Tumaini alifikia hatua ya kwenda kuomba fedha kwa mwanaume aliyewahi kumtongoza, ambapo mwanaume huyo alikubali kumsaidia kwa masharti ya kutembea naye, lakini Tumaini alikataa.

Sehemu nyingine inamuonesha mwanamke aitwaye Magdalena ambaye anaigiza kama mwanamke anayenyanyasika kwenye mahusiano yake akipigiwa mara kwa mara na mchumba wake aitwaye Yann Sow maarufu kwa jina la sanaa kama Emma.

Mwanamke Helen Hartmann maarufu kama Stella yeye na mumewe Alex Temu maarufu kama Ben kwa jina la kisanii kwenye filamu hiyo amewakilisha mateso wayapatayo wanawake wenye changamoto katika afya ya uzazi.

Kama kawaida mwigizaji Godliva ambaye ni kati ya waigizaji wanawake wenye uwezo wa kuuvaa uhusika, amewakilisha kundi la wanawake ambao wana watoto wenye changamoto za kiafya, ameigiza kama mke wa Jonas Mugabe maarufu kama James

Filamu hiyo imefanikiwa kuwa na wahusika wapya kwenye tasnia ya uigizaji hapa nchini tena wenye uwezo, ambapo Seko anasema: ”Tulifanya mchujo kuwapata washiriki ambapo watu kama 300, walipewa kipande cha kuigiza (script) na wakafanya majaribio hivyo wenye uwezo ndiyo walipata nafasi.”

Kati ya waliogiza na kuongeza chachu ni pamoja na Jaji Mkuu wa shindano la kutafuta vipaji la Bongo Star Search (BSS), Ritha Paulsen na mdau wa muda mrefu wa muziki na habari, Sauda Kilumanga.

Madam Ritha ameigiza kama daktari bingwa wa afya ya uzazi, ambapo alikuwa akiwatibu Helen Hartmann maarufu kama Stella na mumewe Alex Temu maarufu kama Ben.

Stella alikuwa akikabiliwa na changamoto ya mimba kutoka kila anapopata ujauzito, alienda na mumewe Ben kwa daktari Madam Ritha, ambapo mbali na kuwahudumia wawili hao, Dk Ritha aligeuka kuwa mshauri wao katika masuala ya afya.

Kwa upande wake, Sauda Kilumanga ameigiza kama mama mzazi wa Magdalena, katika filamu hiyo Magdalena ameigiza kama mwanamke anayeteswa na mchumba wake aitwaye Yann Sow maarufu kama Emma.

Sauda ameicheza vema nafasi yake kama mama ambapo alipelekewa kesi na mwanamwe Magdalena kuwa anateswa, hakuchelewa kumsihi mwanaye huyo kurudi nyumbani haraka asije kuuwawa.

Lakini pia ameigiza kama mwanamke ambaye hakutaka mwanawe apate shida kwenye mahusiano yake hasa pale ambapo alimwokoa wakati Emma alipoenda kufanya vurugu nyumbani.

Ushiriki wa wawili hao kwenye filamu hiyo umegusa hisia za wadau wa filamu hasa kutokana na nafasi zao pia kwenye jamii, wamevaa uhusika vema na kuiongezea thamani tasnia ya filamu.

Binti ni filamu ambayo imeoneshwa kwa mara ya kwanza Siku ya Wanawake Duniani Machi 8 mwaka huu na baadaye itaingiza rasmi kuoneshwa kwenye kumbi za filamu nchini.

Ni kati ya filamu zilizokidhi vigezo vya kuoneshwa kwenye kumbi za filamu kutokana na ubora, imechaguliwa kushiriki kwenye Tamasha la Filamu la PAN nchini Marekani.

Kwa upande wake, Angela Ruhinda alibainisha kuwa, Tanzania inaweza kuwa na filamu bora zaidi zitakazowezesha kushiriki kwenye tuzo za filamu za kimataifa.

Alisema,”Binti imeonesha uwezo wa watanzania kuigiza na hata uwezo wa kutayarisha filamu za kisasa zenye hadhi ya kimataifa, hakika kazi ndiyo kwanza inaanza na tutegemee makubwa zaidi.”

Mwanamitindo mahiri wa kitanzania anayefanya kazi nchini Marekani, Millen Magese akiizungumzia filamu hiyo anasema kuwa ni hatua nzuri kuelekea kwenye uboreshaji wa filamu za Tanzania huku akiisifia kwa namna ambayo imekuwa ya kisasa.

Naye Mwanamitindo Flaviana Matata anasema filamu ya Binti imekidhi viwango vya kimataifa na kuwa ni wakati kwa watanzania kuwekeza kwenye filamu za aina hiyo zenye ubora, ujumbe zinazoweza kuoneshwa kwenye majumba ya sinema ndani na nje ya nchi.

Madam Ritha kwa upande wake anasema kuwa filamu hiyo imemkaribisha kwenye tasnia ya uigizaji na kuwa yupo tayari kuigiza kwenye filamu hasa zenye viwango kama Binti, kwa maana ya filamu inayoweza kuoneshwa katika kumbi za filamu.

Anasema: “Mimi ni mdau wa muziki lakini hii filamu na nyingine nyingi zinazooneshwa kwenye kumbi za filamu kama hizi ni hatua kubwa na yenye kutakiwa kuungwa mkono, kuandaa filamu kama hii iliyochukua mwaka mzima siyo jambo la kawaida hakika ni muda wa kuanza kuwekeza kwenye tasnia ya filamu zaidi.”

Chanzo: www.habarileo.co.tz