Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BABU TALE APIGA MARUFUKU MUZIKI KUPIGWA KWAKE

Babu Tale BABU TALE APIGA MARUFUKU MUZIKI KUPIGWA KWAKE

Sat, 27 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

UKIENDA nyumbani kwa Babu Tale mpaka unaondoka hutosikia mtu anasikiliza muziki humo ndani, hiyo ni kwa mujibu wa Tale mwenyewe, Meneja wa msanii Diamond Platnumz, kiongozi wa lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) na Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Babu Tale anasema kuwa aliamua nyumba yake iwe hivyo kwa sababu anaamini ni mazingira mazuri zaidi kwa ajili ya ukuaji wa watoto wake.

“Sio vibaya kusikiliza muziki na isitoshe ndiyo biashara ambayo imefanya leo hii niwe Babu Tale, lakini naamini kutosikilizwa muziki nyumbani kwangu inakufanya kuwe na mazingira mazuri zaidi kwa watoto wangu, wakikua, wakitoka watasikiliza muziki,” anasema Tale

Anajazia kuwa hata ukiwauliza wanawe hii wanamjua msanii gani hawatakuwa na jibu kwa sababu hawasikilizi muziki kwahiyo hawawajui wasanii pia. Zaidi anatolea mfano kuwa siku moja mtoto wake alikuwa anahojiwa na Zamaradi Mketema, akaulizwa ataje wasanii wa muziki anaowapenda lakini akashindwa kujibu.

“Zamaradi alikuwa haamini kama mwanangu hajui wasanii, akaanza kumuuliza humjui hata Diamond? Mwanangu akasema, Anko Diamond namjua. Unapata picha gani hapo? Wanangu wanawajua wasanii wachache ambao kwetu ni kama familia, hawawajui kama wasanii,” anasema

Tale ameongeza kwa kutaja majina ya wasanii wachache ambao watoto wake wanafahamu kama wajomba kuwa ni Madee, Ben Pol, Rayvanny na Diamond.

KUMKATAA DIAMOND

Kwa sasa inaonekana ni kama vile Babu Tale hayuko karibu na Diamond kama ilivyokuwa hapo awali, ilikuwa kila unapomuona Diamond lazima naye awepo, iwe kushuti video, shoo za nje na ndani, mahojiano na karibu kila mahali.

Kwa sasa mambo ni tofauti, Meneja anayeonekana kuwa karibu zaidi na Diamond ni Sallam SK, kwanini hali iko hivyo? Je Babu Tale amekuwa bosi hivyo ameamua kumuachia Sallam majukumu yake, au ubosi umepungua na nafasi yake imechukuliwa na Sallam au labda ni kwa sababu ya majukumu yake mapya ya Ubunge? Hapa Tale anafafanua hali halisi ilivyo.

“Bora umeuliza, Diamond ni biashara yangu kubwa zaidi, haitatokea siku hata moja niiache. Sijamtenga Diamond, sijapanda cheo, wala kushuka, bado nafanya kazi naye kwa ukaribu sana. Kinachowafanya msinione ni majukumu yangu mapya ya ubunge,” anasema

RAYVANNY KUJITOA WASAFI

Wiki iliyopita msanii Raymond Mwakusa maarufu kama Rayvanny alizindua lebo yake ya Next Level Music ikiwa bado anafanya kazi chini ya Wasafi. Hata hivyo, kumekuwa na tetesi kwamba lebo hiyo ni hatua za awali za Rayvanny kujitoa Wasafi na kwenda kujitegemea, hapa Babu Tale anafafanua.

“Rayvanny hata akisema anajitoa Wasafi sasa hivi sio shida, ndiyo biashara ya muziki ilivyo, leo msanii anakuwa lebo hii kesho lebo nyingine, leo bendi hii, kesho bendi nyingine. Lakini ukweli kuhusu Rayvanny ni kwamba bado yupo sana Wasafi.” anasema.

KASI YA WASAFI

Aidha lebo ya Wasafi imeonekana kuwa na kasi ya 5G kwenye kufanya mambo kiasi kwamba ni kama hata wao wenyewe wamekuwa hawaachiani nafasi ya kutosha.

Kwa mfano, Februari mwaka huu Rayvanny alitoa albamu, kabla hakujapoa Lava Lava naye akaachia EP yenye ngoma nne, kabla EP ya Lava Lava haijashika vizuri mitaani Mbosso akaachia albamu Machi 9 na siku hiyo hiyo Rayvanny naye akazindua lebo yake, na kabla hatujapumua Mbosso ametanga kuzindua albamu yake Machi 20. Hali hii inazua swali la Je, mipango ya WCB kwenye uachiaji wa ngoma ikoje, Babu Tale anafafanua.

“Kwa sasa nchi nyingi zipo kwenye ‘lock down’ au haziruhusu matamasha. Wasafi tunaamini kipindi hiki ni kipindi cha kupanda mbegu. Kwahiyo tunatoa ngoma nyingi kwa sababu tunaamini Mungu atajalia Covid-19 itaisha siku sio nyingi.

ALIKIBA KIROHO SAFI

Katikati ya mazungumzo Babu Tale anagusia kwamba aliona video ya msanii Alikiba akisikiliza na kucheza nyimbo za wasanii wengine wakiwemo wasanii kutoka Wasafi.

Sasa kwa sababu lebo ya Wasafi anayoisimamia Babu Tale inatajwa kuwa na vuta n’kuvute ya muda mrefu na msanii Alikiba, Babu Tale anaulizwa aliipokeaje hiyo ya ngoma zao kusikilizwa na kuchezwa na mpinzani wao.“Naamini katika upinzani lakini nachukizwa na timu, hizi timu timu zinaharibu sana muziki wetu.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz