Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

SIL

Awaua wanawake wawili na kuwalisha nguruwe

Nguruwe Dsss Mkulima mzungu atuhumiwa kuwaua wanawake wawili weusi na kuwalisha nguruwe

Thu, 3 Oct 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kisa cha wanawake wawili weusi wanaodaiwa kupigwa risasi na miili yao kupewa nguruwe wale na mfugaji mzungu na wafanyakazi wake wawili kimezua taharuki nchini Afrika Kusini.



Maria Makgato, 45, na Lucia Ndlovu, 34, inaelezwa walikuwa wakitafuta chakula katika shamba hilo karibu na Polokwane katika jimbo la kaskazini mwa Afrika Kusini la Limpopo mwezi Agosti walipopigwa risasi.

Miili yao ilipewa nguruwe ili kuila katika jaribio la kuondoa ushahidi.

Mahakama sasa itaamua kama itatoa dhamana kwa mmiliki wa shamba hilo Zachariah Johannes Olivier, 60, na wafanyakazi wake Adrian de Wet, 19, na William Musora, 50, kabla ya kesi yao ya mauaji.

Wanaume hao watatu bado hawajaombwa kuwasilisha ombi la dhamana, jambo ambalo litafanyika kesi itakapoanza baadaye.

Katika vikao vya awali vya kesi hiyo, waandamanaji wameandamana nje ya mahakama wakitaka washukiwa wanyimwe dhamana.

Nduguye Bi Makgato, Walter Mathole amesema tukio hilo limezidisha mvutano wa kikabila kati ya watu weusi na weupe nchini Afrika Kusini.

Mivutano ya wazungu na watu weusi imeenea sana katika maeneo ya vijijini, licha ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi miaka 30 iliyopita.

Katika mahakama ya Polokwane, wanaume hao watatu pia wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kumuua kwa kumpiga risasi mume wa Bi Ndlovu, ambaye alikuwa pamoja na wanawake hao shambani – na kesi ya kumiliki bunduki isiyo na kibali.

Hasira za Umma

Mabutho Ncube alinusurika kwenye jaribu hilo, lililotokea jioni ya Jumamosi tarehe 17 Agosti - na kutambaa na kufanikiwa kumwita daktari kwa msaada.

Anasema aliripoti kisa hicho kwa polisi na maafisa waliipata miili ya mkewe na Bi Makgato iliyokuwa ikioza kwenye zizi la nguruwe siku kadhaa baadaye.

Bwana Mathole anasema alikuwa na maafisa wa polisi na aliona tukio la kutisha ndani ya zizi la nguruwe; mwili wa dada yake ulikuwa umeliwa na wanyama hao.

Watatu hao walikuwa wamekwenda shambani kutafuta chakula kutoka katika bidhaa zilizokwisha muda wake au ambazo muda wake wa matumizi unakaribia kuisha. Vyakula hivyo mara nyingi huachwa shambani na hupewa nguruwe.

Familia ya Bi Makgato inasema imesikitishwa sana na mauaji yake - hasa wanawe wanne, wenye umri wa kati ya miaka 22 na mitano.

"Mama yangu alikufa kifo cha uchungu, alikuwa mama mwenye upendo ambaye alitufanyia kila kitu. Hatukukosa chochote kwa sababu yake,” Ranti Makgato, mtoto mkubwa, alisema huku akitokwa na machozi.

"Nadhani nitalala vyema usiku ikiwa wauaji watakosa dhamana," aliongeza.

Chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) kimesema shamba hilo linafaa kufungwa.

"EFF haiwezi kuvumilia wakati bidhaa za shamba hili zinaendelea kuuzwa kwani zinahatarisha afya za watumiaji," kilisema chama hicho baada ya miili hiyo kupatikana.

Tume ya Haki za Kibinadamu ya Afrika Kusini imelaani mauaji hayo na kutaka kuwepo na mazungumzo ya kupinga ubaguzi wa rangi kati ya jamii zilizoathirika.

Vikundi vinavyowakilisha wakulima, ambao mara nyingi ni wazungu, wanasema jumuiya za wakulima zinahisi kushambuliwa katika nchi yenye kiwango kikubwa cha uhalifu - ingawa hakuna ushahidi kwamba wakulima wako katika hatari yoyote zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.

Matukio mengine

Matukio mengine mawili ambayo yamechochea mvutano kati ya wazungu na watu weusi hivi karibuni.

Katika jimbo la mashariki la Mpumalanga, mkulima na mlinzi wake walikamatwa mwezi Agosti kwa madai ya mauaji ya wanaume wawili katika shamba la Laersdrift karibu na mji mdogo wa Middleburg.

Inadaiwa watu hao wawili, ambao miili yao iliteketea kiasi cha kutotambulika, walituhumiwa kuiba kondoo.

Washtakiwa wanaendelea kuzuiliwa huku majivu yakifanyiwa uchunguzi wa DNA.

Kesi nyingine inamhusu mkulima wa kizungu mwenye umri wa miaka 70, anayedaiwa kumgonga gari kwa makusudi mvulana wa miaka sita, kumvunja miguu yote miwili, kwa kuiba machungwa kwenye shamba lake.

Kesi ya Christoffel Stoman, kutoka Lutzville katika jimbo la Western Cape, inaendelea.

Mahakama imeelezwa kwamba mama na mtoto huyo walikuwa wakipita shambani walipokuwa wakielekea mjini kununua mboga.

Inadaiwa mtoto wa miaka sita alisimama kuokota chungwa lililokuwa chini - na mama huyo alitazama kwa hofu huku mkulima huyo akimkanyaga mtoto huyo kwa gari.

Mamlaka ya Kitaifa ya Mashtaka (NPA) ilisema mkulima huyo anakabiliwa na makosa mawili ya kujaribu kuua na kuendesha gari kwa uzembe.

Msemaji wa NPA, Eric Ntabazalila alisema serikali inapinga ombi la mshtakiwa la kuachiliwa kwa dhamana.

Vyama viwili vya kisiasa - African Transformation Movement na Pan Africanist Congress - vinatoa wito wa kunyang'anywa shamba la Bw Stoman kufuatia tukio hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live