Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amber Ruty akosa tena dhamana, atupwa rumande

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Mshtakiwa, Rutyfiya Abubakary maarufu 'Amber Ruty' na mwenzake, Said Bakary Mtopali wameendelea kusota rumande baada ya kukosa watu wa kuwadhamini.

Amber Ruty na Mtopali wameendelea kusota rumande ikiwa leo Jumatatu Novemba 26, 2018 ni siku ya 24, tangu walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  kujibu mashtaka manne likiwemo la kufanya mapenzi kinyume na maumbile.

Washtakiwa hao wanadaiwa kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili kila mmoja na kusaini bondi ya Sh15 milioni.

Pia wadhamini hao, wanatakiwa wawe na vitambulisho vya taifa na washtakiwa hao wasalimishe hati zao za kusafiria mahakamani hapo na kwamba wasitoke nje ya  Dar es Salaam bila ruhusa ya mahakama.

Amber Ruty, Mtopali na mwenzao, James Charles maarufu ‘James Delicious’ ambaye yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana, walifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu, Novemba 2, 2018 kujibu mashtaka yanayowakabili.

Awali, Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono akisaidiana na Faraj Nguka amedai leo Jumatatu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Kombakono amedai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakili huyo baada ya kueleza hayo, Amber Ruty alinyoosha mkono akiwa kizimbani na kudai ana wadhamini.

Wadhamini wa Amber Ruty waliitwa na kujitokeza mwanamke mmoja ambaye hakuwa amekamilisha masharti ya dhamana.

Kwa upande wake mshtakiwa Mtopali, yeye alidai wadhamini wake wapo njiani wanakuja mahakamani hapo.

Hakimu Rwezile baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, amesema masharti ya dhamana yako wazi kwa washtakiwa hao na kama wadhamini hao watafika mahakamani hapo kabla ya saa 9:30 alasiri, wakiwa wamekamilisha masharti ya dhamana, watapata dhamana.

"Ikiwa wadhamini watachelewa hadi muda wa Mahakama unaisha, basi washtakiwa hao watarudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa," alisema Hakimu Rwizile.

Hakimu huyo ameahirisha kesi hiyo hadi, Desemba 10, 2018 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Katika  kosa la kwanza la kufanya mapenzi kinyume na maumbile ambalo linamkabili Amber Ruty, inadaiwa Amber Ruty alitenda kosa hilo kati ya Oktoba 25, 2018 ambapo alimruhusu Said Bakary Mtopali kumuingilia kinyume na maumbile, kosa ambalo amelikana.

Katika shtaka la kufanya mapenzi kinyume na maumbile, linamkabili mshtakiwa wa pili Said Bakary Mtopali ambapo anadaiwa kati ama baada ya Oktoba 25,2018 jijini Dar es Salaam alifanya mapenzi na Amber Ruty kinyume na maumbile.

Kosa la tatu la kuchapisha video ama picha za ngono, linalomkabili James Charles au James Delicious inadaiwa kuwa kati ya Oktoba 25, 2018,  Charles alisambaza video za ngono kupitia makundi ya Whatsapp.

Kosa la nne ambalo ni kusababisha kusambaa picha za ngono linamkabili Amber Ruty na Said Abubakary Mtopali ambapo wanadaiwa kati Oktoba 25, 2018 walisambaza picha za ngono kupitia makundi ya WhatsApp. Kosa ambalo wamesema si kweli.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hayo walikana kutenda makosa hayo .



Chanzo: mwananchi.co.tz