Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ally Choki afunguka kujiunga na Tukuyu Sound, kuirudisha Extra Bongo

ALLY CHOCKY Hj Ally Choki afunguka kujiunga na Tukuyu Sound, kuirudisha Extra Bongo

Tue, 5 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya Ally Chocky kupanda jukwaa la Tukuyu Sound Ijumaa iliyopita na kufanya vizuri sana, mashabiki wengi wa dansi wameanza kutabiri kituo kifuatacho cha mwimbaji huyo.

Siku chache zilizopita Ally Chocky alitangaza kujiengua Twanga Pepeta na kusema anataka kuwa msanii wa kujitegemea.

Lakini baada ya kupanda jukwaa la Tukuyu na kufanya mzaha wa hapa na pale ulioashiria kuwa huenda akajiunga na bendi hiyo, wadau wa dansi wakaingia mkenge na kuamini kuwa Ally Chocky anakwenda Tukuyu Sound.

Lakini wako pia mashabiki kadhaa wanaoamini kuwa Chocky yuko njiani kuifufua bendi yake ya Extra Bongo.

Baada ya mwimbaji huyo kushuka jukwaani, Ijumaa iliyopita pale Mawasiliano Park, Saluti5 ilipata wasaa mrefu wa kuzungumza naye.

Ally Chocky alifunguka mambo mengi sana kuanzia jinsi alivyorejea Twanga Pepeta hadi namna alivyoondoka.

Bahati mbaya sana, Chocky aliomba baadhi ya mazungumzo hususan yaliyopelekea kuondoka kwake Twanga, yasiende hewani kwasasa hadi hapo atakapoamua vinginevyo.

Kikubwa Chocky alisisitiza kuaga wanamuziki wote na viongozi wa Twanga Pepeta na akafafanua kuwa hataki kutengeneza malumbano yoyote na bendi hiyo.

"Namheshimu sana mmiliki wa Twanga, Asha Baraka, nawaheshimu viongozi na wanamuziki wote, nimeondoka bila kumtaja wala kumchafua mtu yeyote, naomba nao waniheshimu na wasinilazimishe kuongea vitu vya kihuni", alisema Ally Chocky.

JE, ANAJIUNGA NA TUKUYU SOUND?

Ally Chocky akaiambia Saluti5 kuwa bado msimamo wake ni kuwa msanii wa kujitegemea.

"Kwa muda huu sina mpango wa kujiunga na bendi yoyote, ninataka kufanya kazi kama msanii mwalikwa iwe Tukuyu, Town Classic, Twanga Pepeta au bendi yoyote ile, mfumo huu utanifanya niwe huru na kupata wasaa wa kutengeneza project zangu binafsi", anafafanua Chocky.

ANAFUFUA EXTRA BONGO?

Chocky amesema atafufua Extra Bongo siku akijiridhisha kuwa sababu zilizomfanya avunje bendi zimeondoka au kupungua.

"Nilivunja Extra Bongo kwa sababu sikutaka 'stress' za kuendesha bendi, kumiliki bendi ni mzigo mkubwa, kwasasa sifikirii hilo jambo, haipo kabisa akilini mwangu, siku nikijiridhisha kuwa mazingira ya biashara yamekuwa rafiki, labda ninaaweza nikakaribisha hilo wazo.

HAONI KUWA KUTOKUWA NA BENDI NI JAMBO LISILO NA AFYA??

Alipoulizwa na Saluti5 kuwa haoni kuwa ni jambo lisilo na afya kwa yeye kutokuwa kwenye bendi yoyote, Chocky alijibu hivi:

"Siku ukifika wakati sahihi, kwa uwezo wa Mungu nitafanya jambo sahihi, kwasasa naridhika na maisha ya kuwa msanii wa kujitegemea".

Chanzo: www.tanzaniaweb.live