Msanii nguli wa muziki wa dansi, Ally Chocky ameshangazwa na ushauri wa msanii mwenzake Mwinjuma Muumini kuhusu Twanga Pepeta.
Chocky amesema Muumini hajawahi kuwa mshauri wake na pia hajawahi kuwa mwema kwa Twanga Pepeta hivyo chochote anachoongea ni sehemu ya roho mbaya na kutapatapa.
"Nimesoma maoni ya Muumini akitaka turejeshe Double Extra na kutaka Twanga isinipokee kwasababu nitakwenda kufunika vipaji vya wasanii chipukizi, ni maoni ya ovyo na yaliyokosa dira," anaeleza Chocky katika mazungumzo yake na Saluti5.
Chocky akatiririka zaidi: "Muumini ametuma watu kadhaa kwangu kuja kunishawishi turejeshe Double Extra, nimewaambia sina mpango wa kutengeneza bendi na mtu aliyekufa kisanii miaka mingi iliyopita.
"Nitafutie hit song ya Muumini baada ya albam ya "Kilio Cha Yatima", huyu mtu zaidi ya miaka 21 hana kazi yenye maajabu, anataka kwenda kufufukia kwenye mgongo wangu.
"Bendi zake zimemshinda mara chungu nzima, kila siku anabadili jina la bendi. Kwasasa hata sijui anamiliki bendi gani.
"Mimi niko Extra Bongo na kama nitaamua kuifunga bendi basi hakuna wa kunipangia pa kwenda wala cha kufanya, kila mtu apambane na hali yake.
"Muumini amepita Twanga Pepeta, atuambie ameacha kazi gani ya maana, wimbo wake upi aliotunga ambao unapigwa kwenye maonyesho ya Twanga? Wengine tunakumbukwa na kuthaminiwa na mashabiki wa bendi hiyo kwa yale tuliyoyafanya."
Kuhusu Extra Bongo, Chocky amesema mambo mazuri yanakuja, watu wakae mkao wa kula na muda si mrefu watapata taarifa ya mwelekeo wa bendi.