Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyedhaminiwa na Diamond asimulia mkasa uliomkuta

29289 Pic+diamond TanzaniaWeb

Thu, 29 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hivi karibuni msanii wa Bongofleva, Naseeb Abdul maarufu kwa jina la Diamond, alimpa udhamini mwanafunzi wa chuo cha uandishi wa habari cha Dar es Salaam School of Journalism (DSJ), Janeth Jastine, baada ya kuguswa na hali yake.

Mwanafunzi huyo anayesomea stashahada ya uandishi wa habari, ana ulemavu wa mguu ambao umekatwa baada ya kugongwa na gari.

Diamond alitangaza kumdhimini mwanafunzi huyo baada ya kumuona katika kipindi cha televisheni akielezea tatizo lilosababisha afikie hatua ya kushindwa kulipa ada.

Ajali yasababisha akatwe mguu

Janeth mwenye umri wa miaka 20, anasema alipata ajali Agosti 24, mwaka 2016 Buguruni Malapa, Dar es Salaam alikokuwa akiishi.

Anasema ajali hiyo ilimpata akiwa amekaa barazani mwa nyumba aliyokuwa akiishi.

Kwa mujibu wa Janeth, siku tukio hilo lilipotokea alikuwa amekaa barazani hapo ambapo lilikuja gari dogo na kumshusha mtu, wakati lilipotaka kuondoka dereva badala ya kurudi nyuma alikanyaga mafuta na kuliendesha kwa kwenda mbele na kumfikia alipokuwa amekaa na kumgonga.

Baada ya hapo anasema alipelekwa Polisi kwa ajili ya kuchukua fomu ya PF3 kisha hospitali ya Amana alikoanza kupatiwa matibabu.

“Amana baada ya kuona hali yangu ni mbaya walinipa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu zaidi,” anasema.

Anasema Septemba 10, mwaka huo, ikagundulika kuwa mguu wake wa kushoto umeharibika kiasi cha kutoweza kutibika ukiwepo ambapo siku mbili baadaye ulikatwa.

Hata hivyo, anasema mguu wake wa kulia licha ya kupata majeraha, lakini hayakuwa makubwa kama ilivyokuwa kwa ule wa kushoto.

“Maumivu niliyokuwa nikiyasikia katika nyonga sikudhani kama siku moja nitaweza kusimama. Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kusimama tena,” anasema.

Alivyoahirisha masomo

Janeth anasema wakati anapata ajali alikuwa stashahada mwaka wa kwanza, hivyo ilibidi aahairishe masomo kwa mwaka mzima mpaka alipopona.

Anasema wakati akipata ajali baba yake ndio kwanza alikuwa amestaafu, na siku mbili baada ya tukio hilo malipo ya mafao yake yaliingia kwenye akaunti ya benki.

Janeth anasema asilimia kubwa ya fedha hizo alizitumia kumtibu kiasi cha kushindwa hata kumalizia ada. Matibabu hayo yalihusisha kumpatia miguu bandia ambayo alibadilishiwa zaidi ya mara mbili kutokana na sababu mbalimbali.

Anasema mguu wa kwanza ulikuwa na tatizo la baadhi ya vifaa vyake kutopatikana madukani kwa kuwa vilikuwa bado viko bandarini, hivyo alishauriwa kwa muda anunue vya kujishikiza vinavyopatikana nchini.

Hata hivyo, anasema kwa kuwa havikuwa vifaa halisi alipata shida kuutumia, hivyo kushauriwa aende Hospitali ya Rufaa ya Kilamanjaro (KCMC) kwa ajili ya kupata mguu mwingine.

“Nilisafiri hadi Moshi kwa ajili ya kufuata mguu mwingine, lakini nao haukuwa msaada kwangu kwani kidonda kilichotokana na kukatwa mguu kilikuwa hakijapona jambo lililokuwa kikwazo kuutumia” anasema.

Alielezwa kuwa inatakiwa aliyekatwa mguu ni lazima apone kidonda ndipo aweze kuvaa mguu wa bandia.

Kutokana na hali hiyo, anasema alilazimika kuweka vitambaa kuukaza ili aweze kuingia darasani.

Baada ya kuutumia kwa muda mguu huo anasema kidonda kilikauka na kumweleza sasa ulikuwa wakati wa kutengenezewa mguu wa kudumu ambapo alisafiri hadi Hospitali ya General mjini Dodoma ambako alitengenezewa anaoutumia sasa.



Chanzo: mwananchi.co.tz