Dar es Salaam. Wadau wa tasnia ya habari wamelaani kitendo cha mwigizaji Irene Uwoya kuwarushia fedha waandishi wa habari wakieleza ni udhalilishaji wa tasnia.
Tukio hilo lililoibua mjadala mzito lilitokea juzi wakati wa mkutano wa wasanii na waandishi wa habari, Uwoya aliwarushia fedha kitendo kilichosababisha vurugu na kuharibika kwa baadhi ya vifaa vya wanahabari.
Tayari Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), leo limewaita Uwoya na Steven Nyerere kuhusiana na tukio hilo.
Katibu wa Basata, Godfrey Mngereza akizungumza na Mwananchi alisema, “kweli tumewataka wafike hapa kesho (leo) kwa ajili ya mahojiano, kutokana na kitendo hicho kilichozua mjadala hapa nchini.”
Akizungumza na Mwananchi Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Rose Reuben alisema kitendo kilichofanywa na Uwoya ni udhalilishaji mkubwa wa tasnia ya habari.
Hoja kama hiyo imetolewa pia na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga aliyeeleza kuwa kitendo hicho kimetia aibu tasnia. “Lazima tujiulize tunakosea wapi kiasi cha kuwafanya wengine watudharau namna hii. Kazi ya uandishi ni muhimu na inategemewa na sekta zingine,” alisema
Pia Soma
- VIDEO: Mrema: Mimi ni nani hata nimkatalie Rais
- Shahidi kesi ya Zitto aeleza alivyowapokea majeruhi wanaodaiwa kumuua polisi
- ATCL kuzindua safari ya Mumbai leo