Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ali Kiba shikilia hapo kwenye U-Mediocre

Aa8d4a6519c52477d23cbc0663d06609 Ali Kiba shikilia hapo kwenye U-Mediocre

Sat, 10 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

You call me Kibaka, They call me King Kiba. Baba Keyaan, Toto la mama Kiba, Njaa mimi nashiba, Unaishi kwa kuniiga, And Am alright, Ushamba mwiko kwa mtoto wa Kariakoo, Sichezi na dada zangu nacheza na dadako, Mixer mkong’oto, We unauza siso, Mimi ndio bishoo……..

Hayo ni baadhi ya mashairi ya wimbo mpya wa Ali Kiba alioupa jina la Mediocre ambao umenifanya ndani ya wiki mbili kutwa mara tatu niwe ‘nina dozi’ ya kuusikiliza kwa umakini na leo nimepata majibu ya kile nilichokuwa nakitafuta ndani yake.

Mashabiki wa muziki na wachambuzi wametofautiana kuna wale ambao wimbo ukitoka tu wanaukubali haraka na kuupatia majibu na kuna wengine, ambao huchukua muda kuutafakari na kuuelewa, mimi kwa wimbo huu nimekaa kundi hilo la pili.

Kiba anatoa wimbo huo ikiwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu mashabiki wake wakiwa ‘wanafurahia’ kuusikiliza wimbo wake mwingine Am so hot ukiwa bado ‘wa moto’.

Wimbo huo ulibebwa zaidi na video yake, ambayo ndani alimtumia Hamisa Mobeto ambaye ni mzazi mwenzake Nassib Abdul, Diamond.

Kwa kipindi kirefu anga la muziki wa Bongo Fleva limekuwa likifukuta kwa kupambanishwa wasanii hawa Diamond na Ali Kiba huku ikionekana Diamond kumzidi mwenzake kwenye baadhi ya ngoma na hata kimafanikio.

Wawili hawa tunaweza kusema wametokea mlango mmoja mpaka hapa walipofika ukifuatilia historia zao za muziki utapata kuna sehemu zinakutana.

Kiba ndiyo wa kwanza kutoka kuliko Diamond kama tunavyojua katika mapambano ya kutoka kimaisha kila mmoja anatumia njia zake za kumpa mafanikio ili kufikia malengo, kigezo cha kuwa wakwanza kuanza hapa huwa hakipo.

Nimekuwa nikisikiliza pande zote mbili za mashabiki wa wasanii hawa wanapotambiana, mashabiki wa Diamond pointi kubwa waliyokuwa wakiitumia kwa kuwaponda wenzao ni kuhusu Kiba kinachomfanya asitoboe kwamba anafanya muziki kistaarabu hali inayomfanya apoe sana.

Kauli hiyo imenifanya niitafakari kwa kipindi kirefu na nikabaini kuwa huenda ni kweli baada ya kumuangalia Kiba na Diamond mwenendo wao wa maisha ya kila siku.

Kuna kauli tunaambiwa ‘kama unaamua kuwa wamoto uwe wa moto kweli na kama ukitaka uwe wa baridi uwe baridi kweli na wala usiwe wa uvuguvugu.’

Ni kweli upande huu Kiba alikuwa hajaufanyia kazi, aliamua kuwa msanii, lakini hakutaka kuwa msanii kweli alitaka kuwa kama shabiki wa msanii.

Katika mahojiano yake Kiba alieleza maana ya neno Mediocre ni mtu au mambo fulani hivi yanayoendaenda au mambo ya ujanja ujanja.

Kwenye makala haya tunasafiri na maana ya Mediocre ni mtu mjanja mjanja anayejua kucheza na alama za nyakati ili kufanya mambo yake yaende kwenye mstari.

Ukimuangalia Kiba kwa sasa amekuwa haswa mediocre tofauti na awali, hii itasaidia kujiweka vizuri katika maisha yake ya kimuziki na hivi ndivyo muziki anavyotaka, msanii anatakiwa awe akilini mwa watu muda wote.

Kwanza kitendo cha kumtumia Mobeto kwenye video yake ni u-madiocre tosha kumemfanya watu wamzungumzie na hata huu wimbo wake wa sasa mashairi yake yote mtaani yamepokewa kama ni kijembe kwa mpinzani wake, achana na ile rangi aliyopaka kichwani.

Kama Kiba ataamua kuendelea na u-mediocre huu ni wazi yule Kiba aliyekuwa akitakiwa na mashabiki wake awe, ndio atakuwa.

Chanzo: habarileo.co.tz