Pichani mwanadada Kayley Stead (27) amelazimika kuendelea na shamrashamra za ndoa/harusi yake ukumbini licha ya bwanaharusi kumpotezea kwa kutotokea siku ya harusi hadi sasa.
Kayley ambaye ni mfanyakazi katika kampuni ya BIMA kutoka Swansea, Uingereza harusi yake ilipangwa kufanyika Septemba 15, mwaka huu.
Imeelezwa kuwa, wawili hao walikuwa pamoja kwa miaka minne katika mahusiano ambapo walichumbiana mwaka 2020 na hawakuwahi kuwa na ugomvi hata ndoa ilipokaribia.
Kukaribia ndoa, mama mkwe wake mtarajiwa (mama wa mwanaume) alimwambia Kayley bwanaharusi hataonekana siku ya ndoa atakimbia na kweli hakuonekana.
Siku ya harusi hadi saa tano asubuhi mrembo huyo alishapambwa kila kitu lakini alipompigia simu baba mkwe akaambiwa bwanaharusi kawasiliana nae ila hatokuja kwenye tukio.
Kayley alichanganyikiwa kwa sababu hata akiba yake aliyojiwekea siku nyingi aliamua kuitumia katika maandalizi ya harusi yake kuinogesha zaidi. Alitumia £12,000 ambazo ni zaidi ya Tsh milioni 31 na kila kitu kilikuwa tayari.
Baada ya kuwaambia watu kilichotokea kuwa bwanaharusi hajibu simu zake, videographer alitania kwamba kwa nini tusiendelee tu na harusi bila bwanaharusi maana tayari gharama kubwa zimetumika na wageni tayari wapo ukumbini.
Baadhi ya wengine walikubaliana na hilo na Kayley akakubali kuendelea na sherehe ya harusi bila mwanaume ingawa wapambe wa mwanaume nao walikuwepo lakini hawakujua alikokuwa bwanaharusi tangu usiku wa kuamkia ndoa/harusi.
Kayley na wapambe wake walijumuika na wapambe wa bwanaharusi na wageni wakaingia ukumbini kwa mbwembwe zote huku wakicheza wimbo wa Lizzo unaitwa Good As Hell, walikula, kupiga picha na mengineyo ya kiharusi.
Upande wote wa bibi harusi ulikuwa ukumbini kumfariji wakiwemo kaka zake na baba yake mzazi kwani ilikuwa Ndoto Kayley kucheza muziki na baba yake siku ya harusi yake
Kwa sasa Kayley ameikubali hali ya kuwa single kwani tangu hapo hakutafutwa na mwanaume hata kumueleza tu sababu ya kumtia aibu aliyomfanyia.
Kuhusu fungate, wawili hao walipanga kwenda kulila nchini Uturuki lakini fungate limeshindwa kutokea baada ya harusi asilia kuota mbawa.
Kayley amesema hataki kuikumbuka siku hiyo Kama ya huzuni kwake ila kama ya furaha kwa sababu ya yale mazuri yaliyotokea ukumbini ikiwemo kukata keki, kucheza, kupiga picha.