Ukitazama nyota kama Toni Braxton (56), Mariah Carey (54), na Taraj P. Henson (53), ni vigumu kuamini kwamba warembo hawa wana zaidi ya miaka 50. Hata hivyo, siri yao inaweza kuwa ni jinsi wanavyojitunza na kuishi maisha yao, hali inayowafanya waendelee kuonekana kama mabinti wadogo.
Inawezekana kabisa kuwa wapo watakaopinga kuwachukulia hawa mastaa kama mfano, wakidai kwamba wako katika mataifa yaliyoendelea na wanaweza kumudu kufanya kila wanachohitaji ili kujiweka sawa na kupata mwonekano unaovutia.
Lakini cha ajabu, hata hapa Tanzania tunao Watanzania wenzetu wanaojali miili yao pia. Wapo watu kama Millen Magese (44), Faiza Ally (40), Irene Kiwia (44), Ritha Paulsen (47) na wengineo.
Licha ya umri wao kuwa mkubwa, wanaendelea kuwa na mwonekano wa kuvutia kana kwamba ni wasichana wadogo.
Dhana kwamba wazee wanapaswa kujiweka mbali na masuala ya urembo inaweza kuwa na ukweli fulani, lakini uzito kupita kiasi ni tatizo linaloharibu mwonekano wa wanawake wengi, na sasa hata wasichana wadogo wanakumbwa na kadhia hiyo.
Mwanahabari Salma Msangi amekuwa akihoji mwenendo wa wasichana na wanawake wenye umri mdogo kuonekana kama watu wazima zaidi kuliko baadhi ya wanawake wenye umri mkubwa.
Katika mahojiano na jarida hili, Salma anasema kuna shida kubwa katika malezi ya vijana wa sasa, ambayo yamesababisha watoto kufikiria kuwa na uzito ni ishara ya afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amekuwa akilizungumzia hili kila mara na ameendelea kutoa wito kwa wazazi kutofurahia watoto wao kuwa na uzito kupita kiasi, akisema ni hatari kwa afya.
Anasema kuwa na uzito mkubwa kunaweza kusababisha matatizo ya kiafya kwa watu wa umri wowote ule. Profesa Janabi anasema hata watoto wachanga wanaweza kuathiriwa pia.
Kujitambua na kuithamini afya
Salma Msangi (40) anasisitiza kwamba tatizo kubwa ni watu kutojitambua, anasema hii inaweza kusababisha kushuka kwa thamani ya miili yao.
Anasema hivi sasa mabinti wengi wana umri mdogo, lakini kwa mwonekano wao unaweza kusema ni wazee, kwa sababu hawana mfumo mzuri wa maisha, hawazingatii lishe bora, wanakula hovyo, hawapati muda wa kutosha kupumzika, wengine walevi, wanatumia vipodozi vyenye kemikali, miili yao wanaichosha kwa kutumika hovyo halafu bado wana msongo wa mawazo.
Kwa mwenendo huo kuzeeka ni lazima, lakini wapo watu wazima ambao wana mfumo mzuri wa maisha wamechagua kujipenda na kujithamini ndiyo maana wanaonekana kana kwamba ni wasichana wadogo. Nikijitolea mfano mimi nina miaka 40, ni mama wa watoto watatu, mke, dada na nina majukumu mengi ya kifamilia, lakini nimechagua kujipenda na kujithamini kwanza. Wapo wanaoniambia mbona upo kama hujazaa, kiukweli nashindwa kuelewa uhusiano wa kuzaa na kujizeesha. Tunapaswa kuelewa kuwa ni muhimu kuishi kwa kuzingatia afya.
Mazoezi yanavyochangia
Mwalimu wa mazoezi ya viungo, Godfrey Mkinga anasema licha ya mazoezi kuwa na mchango mkubwa katika kuufanya mwili kuwa imara, pia ni kinga dhidi ya magonjwa, hivyo ni muhimu kwa kila mtu kufanya mazoezi kila mara.
“Hakuna sababu inayomfanya mtu asifanye mazoezi, iwe mjamzito, mama anayenyonyesha au hata mzee, watu wote wanapaswa kufanya mazoezi kuwa sehemu ya maisha. Si lazima mazoezi yawe ya kupunguza uzito pekee, ndiyo maana nasema kwa kila hali hupaswi kukwepa, hata wajawazito wana mazoezi yao ambayo ni muhimu katika safari ya kuleta kiumbe duniani.
“Wasichofahamu wengi ni kwamba kadiri umri unavyokwenda, uzito wa mwili unapaswa kupungua sio kuongezeka, sasa kama wewe unajiona kwa vile ni mama basi unatakiwa kujiachia tu, utakuwa hauutendei haki mwili wako.
Anasema faida za mazoezi ni pamoja na kuukinga mwili dhidi ya maradhi yasiyoambukiza, mwonekano mzuri wa mwili, pumziko la mwili na akili, hasa baada ya kazi ambayo huongeza uwezo wa kufikiri.
Faida nyingine anasema ni kuiwezesha akili kufanya kazi kwa haraka, kuongeza hamu ya kula na kumwezesha mtu kuwa na wepesi katika ufanyaji wa maamuzi sahihi kwa haraka.
Shilwa Mboma (46)
Siku zote siruhusu kukasirika kutawale kichwa changu, huenda hiyo ikachangia kunifanya nionekane bado niko imara, licha ya kuwa umri wangu unazidi kusonga na ni mama wa watoto watatu tena wakubwa.
Huwa nakwepa kuweka vitu moyoni na furaha ndiyo kipaumbele changu, hivyo najitahidi kufanya yale yanayonifanya nifurahi au kujiweka katika mazingira yanayoweza kunipatia furaha.
Sifanyi mazoezi, nazingatia mlo kamili, ingawa kuna vitu wakati mwingine nateleza kwenye suala la chakula, lakini najitahidi niwe na kiasi kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa na wataalamu wa afya.
Kingine najitahidi kujiweka mbali na vitu vinavyoweza kuwa hatari kwa afya, sijawahi kunywa pombe wala kilevi cha aina yoyote ile na wala situmii sigara.
Angella Michael (45)
Anakataa dhana kwamba umri au kuzaa ndiyo sababu ya kuzeeka. Anaamini watu wengi wanajichosha wenyewe kwa kula na kunywa vibaya. Kwa kudumisha mlo kamili na kufanya mazoezi, anasisitiza kwamba anadhibiti uzito wake na anaweza kuonekana kama bado yuko kwenye umri mdogo. Anahimiza wanawake kubadili mtindo wa maisha, kula vizuri na kuepuka vitu vinavyoweza kuathiri afya na mwonekano wao,
Kwa kuhitimisha, ni wazi kwamba kuzeeka sio tu kunahusu umri wa kalenda, bali ni jinsi unavyojiweka na junavyouhudumia mwili wako.
Kujitambua, kujithamini, mazoezi na lishe bora ni mambo muhimu katika safari ya kupambana na umri mkubwa ambao vijana wa mjini wanaita ‘Age go’ na kubakia katika mwonekano unaovutia muda wote.