Kwa muda wa wiki mbili sasa kumekuwa na minong’ono ya vita vya maneno baina ya uongozi wa lebo ya muziki ya Konde Music Worldwide na wasanii Cheed na Killy kuhusu kukatishwa kwa mkataba wao pale.
Ikumbukwe Okotba 10, kiongozi wa lebo hiyo, Harmonize alitangaza kukamilika kwa muda wa wawili hao katika lebo hiyo na haka kuwatakia kila la kheri katika maisha yao ya muziki kama wasanii huru.
Wengi walijua kuwa wawili hao waliondoka kwa Imani sawa ila baadae kukaibuka taarifa mpya kabisa kwamab wameonekana kweney makao ya BASATA wakimshtaki Harmonize kwa kile walisema ni kutimuliwa Konde Gang kwa njia isiyofaa.
Sakata hilo ambalo linaendelea baina ya Cheed na Killy pamoja na aliyekuwa bosi wao Harmonize limevutia maoni kinzani kutoka kwa baadhi ya wadau katika Sanaa ya muziki lakini pia wasanii wenzao.
Wikendi, chawa wa WCB Wasafi aliwashauri kukoma kupelekana na kesi za kumshtaki Harmonize na badala yake wajikusanye na kuangalia mwafaka wa taaluma yao kimuziki. Aliwataka kurudi kwa aliyekuwa bosi wao wa zamani, Alikiba na kuomba msamaha waruhusiwe kurudi pale.
Ikumbukwe Cheed na Killy miaka kadhaa nyuma walikuwa na mkataba katika lebo ya Alikiba, Kings Music ambapo walikatisha na kufuata maslahi mengine kwenye lebo mpya kipindi hicho, Konde MusicWorldwide.
Abdukiba ambaye ni kakake Alikiba na pia mmoja wa wasanii ambao mpaka sasa wamedumu kwenye mkataba na lebo ya kakae akizungumza na wanablogu jijini Mtwara baada ya tamasha la Fiesta alizungumzia kuhangaika kwa wasanii hao wawili.
Kulingana na Abdukiba, Killy na Cheed waliondoka Kings Music kwa ajili ya kutafuta maslahi ambayo kule kwingine walikokimbilia pia kumebuma.
Alisema kwamba wawili hao wanakurupukia tu maisha ya muziki na kuwa wanatafuta kamseleleko, kuteleza kwa ganda la ndizi pasi na kutia bidi katika muziki, na ndio maana wameshindwa kutusua maisha kimuziki katika lebo hata moja.
“Nadhani wenzangu waliangalia maslahi ambayo waliona yanawaruhusu kutoka Kings kwenda Konde Gang. Nahisi hawajaondoka ila uongozi umewapa ruhusa ya kufanya maisha mengine.
"Mimi najua maisha ni magumu sana, wao nahisi labda kwa kauli nyepesi kuna vitu wameviharakia wanavitaka. Halafu tena kwenye maisha hakuna kitu kinakurupua na kua, ni lazima viende hatua kwa hatua ndio viwe,” Abdukiba alisema.