Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AIBU: Fid Q, Tale, Fella wakubwa wanaovuana nguo mbele ya watoto

32532 Fid+pic Tanzania Web Photo

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

NOVEMBA 19, mwaka huu, mtandao ulichafuka kwa maneno ya shombo. Said Fella ‘Mkubwa’ na Hamis Taletale ‘Babu Tale’, walifanya ile kitu inaitwa “Tupa jiwe gizani, ukisikia yalaa ujue shabaha ni asilimia 100.”

Hata hivyo, Mwinjuma Muumini ‘Kocha wa Dunia’ aliwahi kuonya tabia ya kutupa jiwe gizani, linaweza kumpata mama mkwe. Maana unaweza kusikia “yalaa”, halafu anayelia hivyo ni mama mkwe. Utanyang’anywa jiko na chakula bado kuiva.

Tale na Fella wakafyatuka; Ooh, msanii mkubwa wa Hip Hop Kiingereza kiingi kumbe hata gari hana. Kwa msisitizo wenye kubebwa na mshangao wakahoji “Hata Passo?” Tunajua Toyota Passo ni gari dogo bei poa. Huyo mbabe wa Hip Hop anasemwa hana hata Passo.

Wakaenda mbali zaidi, wakasema huyo msanii wa Hip Hop anatakiwa kununua sabuni ili atoe chunusi. Tale akaweka ‘hashtag’ kibao, “#nunuasabuniutoechunusi”. Maswali yakawa lukuki, huyo galacha wa hip hop anayesakamwa ni nani?

Novemba 20, yaani siku iliyofuata Underground King wa Mwanza, Fareed Kubanda ‘Fid Q’, akaibuka na kuandika waraka mrefu kwa Tale, akionesha masikitiko yake kuhusu namna ambavyo anashambuliwa. Fid Q ni fundi-stadi wa Hip Hop. Mpaka hapo una swali?

Tale alijitetea kuwa hakumtaja mtu, lakini akasema lilikuwa jiwe gizani. Na kanuni ni ileile kuwa mwenye kusema “yalaaa” ndiye limempata. Fid Q ndiye alipiga yalaa. Fella alisema, Fid Q aliomba msamaha, kwa hiyo mambo yaliisha.

Majibu ya Tale na Fella yalikuwa kipimo kuwa Fid Q ndiye alilengwa. Awali, Tale alitishia kumtaja jina huyo mkali wa Hip Hop asiye na gari hata Toyota Passo na mwenye chunusi. Fid alipotokeza na kujibu, Tale hakutaja tena jina. Mbona hakusema sio wewe Fid, niliyemkusudia ni fulani?

Hata hivyo, lipo swali; Wanaume wazima kumshambulia mwenzao kuwa hana gari, huo ndio uanaume gani? Mwanaume unataka mwanaume mwenzako awe soft, wewe chunusi za mwanaume mwenzako zinakuhusu nini?

Haifai kwa wanaume kuazima nyodo za kinadada. Wao ndio husema “simtaki mwanaume asiye na gari”, utasikia “aku yule mkaka ana chunusi hata simtaki”. Swaga za kike kuchukuliwa na wanaume. kisha wanaume kuwaambia wanaume wenzao ni janga la Kidaslam.

SEMA FID ALIPANIKI

Hivi karibuni Fid Q ameibuka na gari mpya, Jeep Cherokee 65. Gari matata sana. Bei yake ni kubwa na unaweza kununua Passo zaidi ya 10. Ukilitazama juujuu unaweza kulifananisha na Jeep Patriot ambalo Salha Israel alizawadiwa aliposhinda Miss Tanzania 2011, ila la Fid ni Cherokee. La Salha tuliambiwa ni Sh 70mil.

Zingatia tu kwamba Jeep Cherokee ni bei mbaya kuliko Patriot. Hata hivyo, Fid hajasema kama gari lake ni mpya au mtumba. Maana kuna Cherokee mitumba bei ya manunuzi, usafirishaji jumlisha na kodi, unaweza kufika mpaka Sh 35 Milioni. Kama ni mpya basi ni biashara ya kupita Milioni 100.

Jeep Cherokee la Fid ni rangi ya blue. Lina muziki wa kiwango cha juu. Mwenyewe anasema, mabishoo wengi wana magari, lakini hawana muziki. Amefunga mashine ya Vino Player. Anasema yeye haliiti Jeep, analiita VPR (Vino Player Ride). Yaani Usafiri wenye Vino Player.

Fid anagoma kutaja hata gharama aliyotumia kuvuta hiyo ndinga, lakini swali linakuja, mbona amepaniki? Kwa nini yeye kama mgumu wa Hip Hop asingepotezea maneno ya kejeli kuwa hana gari? Mtu mzima ukiletewa utoto nawe unatakiwa kujibu utoto?

Kiukweli, maneno ya Tale na Fella, kisha majibu ya Fid, ni dhahiri hawa ni watu wazima ambao wameamua kuvuana nguo mbele ya watoto. Vijana wapya kwenye muziki wajifunze nini kwao, ikiwa wenyewe ndiyo kwanza wapo ‘bize’ kuoneshana sanaa za magari, utadhani kumiliki gari ndio kupatia maisha.

HEBU TUSEME NA FID

Vipi kuhusi chunusi na gari? Fella na Tale hawakumtaja jina, yeye alijuaje ni yeye? Nimefanya mahojiano na Fid Q ili aweke haya mambo katika mstari mnyoofu.

FID Q: Nilijua wamenilenga mimi kwa sababu maneno yao yalidhihirisha mlengwa ni mimi. Hata mashabiki walijua ni mimi kwa sababu kila walipopost, mashabiki walinitag. na lile halikuwa jiwe gizani.

SWALI: Haya mambo ya migogoro kati ya wasanii wao kwa wao au baina ya wasanii na wadau wa sanaa, kwako inakupa tafsiri gani?

FID Q: Muziki wetu umetokea sehemu ambayo ulikuwa unaonekana ni uhuni. Kuvaa makoti makubwa jua kali, mabuti makubwa. Kuanza migogoro, hatutaendi mbele.

SWALI: Kuna bifu kati yako na Tale au Fella? Chanzo cha bifu ni nini?

FID Q: Kwanza mimi siwezi kuliita ni bifu. Naita ukurupukaji. Chanzo cha ukurupukaji ni mimi kutoa tangazo la shoo ya Fiesta, sasa wao wakaona naliponda tamasha lao la Wasafi wakati haikuwa kweli. Tanzania matamasha ni mengi. Na maneno ya udambwidambwi kwa ajili ya kupamba shoo ni vitu vya kawaida.

SWALI: Ulipokea vipi kuambiwa una chunusi ununue sabuni?

FID Q: Niseme ukweli wamenikera sana. Mfano Fella ni diwani. Naamini anaongoza watu wengine kule kwenye kata yake ya Kilungule, Mbagala, wanafanana na mimi. Je, anajisikiaje kuongoza watu wenye sura ngumu kama mimi anayenishambulia? Hawajatumia busara.

SWALI: Umeonyesha gari lako mpya, vipi umenunua baada ya kusemwa huna hata Passo?

FID Q: Magari ni vitu ambavyo nimekuwa navyo kwa muda mrefu. Sema tu mimi sio mtu wa kujionesha. Nimesikitishwa na maneno yao kuwa msanii mkubwa sina hata Passo. Mafanikio sio Passo au kuwa na gari. Maneno yao yamenipa wazo la kuandika ngoma ya kueleza maana ya mafanikio.

SWALI: Yapo maneno kuwa unalelewa. Hayo pia unayajibu vipi?

FID Q: Watu wanavyoona baby mama wangu ni Mzungu wanadhani nalelewa. Nawaruhusu wafuatilie Western Union hasa pale Mlimani City waambiwe. Mimi nikienda pale nakwenda kutuma pesa. Silelewi, nalea. Katika Mwanza Mwanza niliimba “Ninavyoishi ki hard core watu nadhani nimepigika”, hiyo ni ngoma ya 2005.

SWALI: Mbona ulikuwa hujionyeshi lakini baada ya kusemwa huna gari umeamua kuliweka gari lako hadharani?

FID Q: Sijapaniki, nimeamua kufanya hivi ili kulinda heshima.

Najua kuna watu nimewakera kwa uamuzi huu, nawaomba sana msamaha.



Chanzo: mwananchi.co.tz