Rapper Curtis James Jackson “50 Cent” amekiri kuwa alikataa ofa ya kulipwa dola za Kimarekani milioni tatu ( 3,000,000 $) ambazo ni zaidi ya Bilioni nane za Kitanzania, iwapo angekubali kushiriki katika Kampeni za Mgombea Urais wa Marekani Donald Trump.
Kwenye mahojiano na Power 105.1 New York, 50 alisema pia alialikwa kutumbuiza wimbo wake maarufu "Many Men" kwenye mkutano wa Kitaifa wa Republican (RNC) July 2024 lakini kwa sababu hapendi kujihusisha na kampeni za kisiasa aliamua kutoendelea na mazungumzo ya kupokea ofa hiyo.
50 Cent alieleza kuwa amekuwa akiepuka kujiingiza kwenye masuala ya siasa kwani kujihusisha na siasa kunaweza kumuweka Mtu katika migongano isiyo na ulazima huku akimtolea mfano Rapper mwenzake Kanye West ambaye alijikuta katika mvutano mkubwa baada ya kutoa kauli za kisiasa.
Rapa huyo alihitimisha kwa kueleza msimamo wake wa kubaki mbali na siasa na kusema kuwa anaamini kujihusisha na masuala haya kunaweza kudhoofisha taswira ya Wasanii.
Kauli hii ya 50 Cent imekuja wakati Marekani ikishuhudia Mgombea Urais Kamala Harris akiungwa mkono na Wasanii kama Eminem, Beyonce, Kelly Rowland, Taylor Swift, Ariana Grande, Cardi B, GloRilla, Jennifer Lopez, Jermaine Dupri, John Legend, Katy Perry, Lil Nas X, Marc Anthony, Rapper Quavo, Stevie Wonder na wengineo.
Mgombea Urais Donald Trump naye ameungwa mkono na Wasanii mbalimbali wakiwemo Kid Rock, Amber Rose, Chris Janson, Jason Aldean na Azealia Banks.