Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara imeahirisha tena kesi ya mauaji inayowakabili maafisa saba wa polisi mkoani Mtwara, hadi itakapotajwa tena Aprili 19, 2022.
Washitakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara leo Jumanne ya Aprili 5, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Mussa Essanju.
Akiahirisha kesi hiyo, Hakimu Mkazi Essanju amesema upelelezi wa kesi hiyo namba 1/2022 haujakamilika.
Amesema watuhumiwa walipopewa nafasi ya kujieleza wamedai kutokuwa na hoja yoyote ya kuiambia mahakama.
Kesi hiyo inawakabili maafisa saba wa polisi wakituhumiwa kumuua mfanyabiashara wa madini Musa Hamis Hamis (25) Januari 5, 2022.
Watuhumiwa hao ni ni Ofisa Upelelezi Wilaya ya Mtwara, Gilbert Kalanje, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Charles Onyango, Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Charles Kisinza na Mkaguzi wa Polisi, John Msuya.
Wengine ni Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi, Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi, Shirazi Mkupa na Koplo Salum Juma Mbalu.
Awali, washitakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Januari 25, 2022 na kusomewa shitaka la mauaji ya kukusudia.
Kama kawaida washitakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo wakiwa chini ya ulinzi mkali na kufunika nyuso zao huku ndugu na jamaa wakifurika kusikiliza shauri hilo.