Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizkid na wenzake wanne kortini

51405 Pic+wizkid

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Washtakiwa watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka  la kuchapisha picha za utupu katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp kisha kuzisambaza.

Waliofikishwa mahakamani ni ni Oscar Urio (30) maarufu Wizkid ambaye ni fundi na mkazi wa Nkuhungu  jijini Dodoma, mfanyabiashara Don Godfrey (36), mfanyakazi wa benki William Kimaro (35) mkazi wa Ubungo,  Feisal Mohamed (27) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Ilala na Abdulrahman Muhidini (34) ambaye ni Wakala wa usafirishaji na mkazi wa Temeke.

Akiwasomea mashtaka wakili wa Serikali, Jenifer Massue, amedai leo April 9, 2019 mbele ya hakimu  Augustina Mmbando, kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka hilo kinyume na sheria ya mtandao.

Massue amedai kuwa katika shtaka la kwanza, ambalo ni kuchapisha picha za utupu linalomkabili Urio, anadaiwa kutenda  kosa hilo Aprili 4, 2016 ndani  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Urio, anadaiwa siku ya tukio alichapisha picha za utupu kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp, huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Massue ameendelea kuwa mshtakiwa wa pili hadi wa tano, kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 5, 2016 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka linalowakabili wamekana na wakili Massue amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mmbando amesema dhamani ipo wazi na kutaja masharti kuwa kila mshtakiwa awe na mdhamini mmoja   kutoka taasisi inayotambulika kisheria atakayesaini hati yenye thamani ya Sh5 milioni.

Pia, wadhamini hao wametakiwa kuwa na vitambulisho vya kazi kutoka taasisi wanazofanyia.

Washtakiwa hao wamefanikiwa kukamilisha masharti hayo. Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 9, 2019 itakapotajwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz