Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wingu zito mhandisi aliyejinyonga Chunya

63801 Mhandisipic

Sat, 22 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Chunya. Bado watu wanajiuliza maswali. Ni sababu gani zilizomfanya aliyekuwa mhandisi wa Halmashauri ya Chunya, Mbeya, Aswile Msika kuchukua uamuzi wa kujinyonga hadi kufa kwa kutumia nguo zake kwa kujitundika juu ya mti bila kuacha ujumbe wowote?

Mwili wa Msika uligundulika juzi wa mchana ukining’inia kwenye mti kando ya barabara inayoelekea Mlima Nnjiwa. Inadaiwa kuwa mtumishi huo alitoweka nyumbani kwake tangu Jumatatu iliyopita kabla ya mwili wake kuonekana katika eneo hilo.

Taarifa ya Polisi Mkoa wa Mbeya inasema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa huenda Msika alichukua uamuzi huo kutokana na msongo wa mawazo kwa kuwa alikuwa anakabiliwa na kesi mahakamani akituhumiwa kupokea rushwa ya Sh1 milioni.

Akizungumzia tukio hilo, Joshua Mlambalala ambaye ni mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni-Chunya, ambako Msika alikuwa akiishi alisema alipewa taarifa za kutoonekana kwake siku moja kabla ya kifo chake.

Alisema mke wa marehemu ndiye aliyemuambia. Alisema mke huyo alimweleza kuwa mumewe alimpigia simu akimtaarifu kwamba ameondoka nyumbani kwenda kuweka mafuta kwenye gari lakini baada ya hapo hakupatikana tena kwenye simu hadi ilipogundulika amefariki.

“Nilikuwa namfahamu vizuri sana kijana yule. Kwa kweli hakuonyesha dalili zozote kwani licha ya kuwa na tuhuma hizo pamoja na mwenzake, yeye ndiye alikuwa mshauri mkubwa wa mtuhumiwa mwenzake ambaye ndiye aliyeshikwa na Takukuru alisema,” Mlambalala.

Pia Soma

Alisema katika jitihada za kumtafuta hapakuwa na dalili zozote kama Msika alikuwa na mtu mwingine mpaka alipokutwa akiwa amejinyonga.

Dada wa marehemu, Edda Mbwaga alisema kwa mujibu wa maelezo aliyopewa na wifi yake, hakuna kitu chochote alichokizungumza kabla ya kifo chake na hakuwahi kuonyesha dalili zozote zile za tofauti.

Alisema, “bado tupo njia panda hatujui kilichomfanya kaka yetu achukue uamuzi wa kujinyonga, na hatujui kama kweli kajinyonga mwenyewe au kuna kitu kingine nyuma yake hatujui…. kwani hakuna ujumbe wowote pengine aliuandika. “Lakini pia hakuna mtu yeyote aliyeonekana kushuhudia tukio hilo wakati akijitundika lakini sote tulipata tu taarifa kwamba nyumbani hayupo na baadaye tukapata taarifa kuwa amejinyonga.”

Mmoja wa marafiki wa Msika ambaye hakutaka kuandikwa jina lake alisema mara zote walizoea kukaa baa moja na kunywa pombe lakini siku zote alikuwa ni mtu wa kawaida isipokuwa siku za karibuni.

Alisema siku tatu kabla ya kifo chake, alionekana kuongeza kilevi lakini hakuna aliyehisi chochote kutokana na mabadiliko hayo.

Marehemu alisafirishwa jana kutoka Chunya na kwenda nyumbani kwao Wilayani Rungwe ambako maziko yalifanyika jana hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz