Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wimbi lasababisha kifo cha mvuvi baharini

Baharinipic Wimbi lasababisha kifo cha mvuvi baharini

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mvuvi mkazi wa Kata ya Rahaleo, amefariki dunia baada ya kupigwa na wimbi kubwa la maji, hivyo kushindwa kuogelea alipoenda kufuata mtumbwi wake katika Bahari ya Hindi, Pwani ya Mikumbi mkoani Lindi.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Lindi, Mrakibu Msaidizi Joseph Mwasabije amemtaja mvuvi huyo kuwa ni Hussen Ahmed (45), mkazi wa Mikumbi.

Amesema tukio hilo limetokea jana Januari 22, 2024 saa sita mchana.

Kamanda Mwasabije amesema mvuvi huyo alikuwa anaenda kufuata chombo chake cha uvuvi kwenye maji, ndipo mawimbi makubwa yakamzamisha akashindwa kuibuka.

"Wavuvi wenzake waliingia majini kumsaidia lakini ilishindikana ndipo walipopiga simu kwetu (Zimamoto na Uokoaji) kuomba msaada," amesema Kamanda Mwasabije.

Amewataka wavuvi katika kipindi hiki cha mvua kufuatilia maelekezo yanayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).

Kwa kufanya hivyo amesema watajua hali ya bahari ikoje hivyo kuepuka madhara.

"Wavuvi wajitahidi kuangalia au kufuatilia hali ya hewa, hili litawasaidia katika kazi zao za uvuvi, ukichukulia hivi sasa ni kipindi cha mvua," amesema.

Pia ametoa wito kwa wazazi kuacha tabia ya kuruhusu watoto kwenda kucheza ufukweni mwa bahari peke yao.

"Wazazi wawe makini na watoto wao, siku kama tatu zilizopita tulipigiwa simu watoto wameingia kucheza baharini wakashindwa kutoka, tuliwahi eneo la tukio kwa bahati nzuri tuliwawahi," amesema.

Mariamu Jumbe, aliyeshuhudia tukio la mkazi wa Mikumbi kuzama, amesema walikuwa wakipita njiani wakamuona akiingia baharini, lakini ghafla walimsikia akiomba msaada.

Amesema wenzake walipoenda hawakumuona.

“Tukio hili limenishangaza, muda si mrefu tumemuona mtu ameingia kwenye maji, ghafla amekufa. Tunashukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoji kwa juhudi walizofanya hadi kuupata mwili wa marehemu,” amesema Mariamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live