Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Lugola amaliza mzozo ndugu waliosusa maiti

14678 MWILI+PIC TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Familia iliyokuwa imeususa mochwari mwili wa ndugu yao, Salum Kindamba jana ilibadili uamuzi na kuamua kuuzika baada ya kushauriana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Familia hiyo iliususa mwili huo mochwari ya Hospitali ya Taifa Muhimbili tangu Agosti 11 huku ikisisitiza kutozika hadi itakapopata majibu ya kilichosababisha ndugu yao auawe.

Awali, familia hiyo ililishutumu jeshi la polisi kwa kumpiga risasi ndugu yao na kusababisha kifo chake.

Soma zaidi: Polisi waitaka familia iliyosusa mwili mochwari kwenda kuuchukua

Lakini, msemaji wa familia, Issa Khalfan Issa aliliambia Mwananchi kuwa wameamua kuzika baada ya kushauriana kwa kina na Waziri Lugola.

Alisema walipofika juzi ofisini kwa waziri huyo walishauriana na kisha akawaomba wasitishe mgomo huo kwa vile alikuwa katika hatua za mwisho kulitafutia ufumbuzi suala lao.

“Kwanza napenda kuwashukuru sana watu wa Mwananchi kwa namna mlivyotupa uwanja wa kupaza sauti na hatimaye dunia ikajua kilio chetu. Sasa tumemaliza mgomo wetu na hapo tupo hatua za mwisho kwenda kumpumzisha ndugu yetu,” alisema.

Soma zaidi: Familia Dar yasusa maiti ya ndugu Muhimbili, yalia na Jeshi la Polisi

Mwili wa Salum uliachwa mochwari kwa muda wa siku 19 huku familia ikisisitiza kuendelea na mgomo huo hata kama ungekaa mwaka mmoja.

Mwananchi ilifika nyumbani kwa kaka wa marehemu eneo la Karakata na kushuhudia jeneza lililobeba mwili wa marehemu likitolewa nje na kisha kusindikizwa hadi msikitini na baadaye katika makaburi ya Karakata, Kipawa.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia, Waziri Lugola ameahidi kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo siku chache zijazo na atafanya hivyo baada ya kupokea ripoti kutoka katika timu yake inayofuatilia suala hilo.

 Soma zaidi: Familia zaendelea kuomboleza miili ikiwa mochwari

“Kwanza tumpongeze waziri kwa namna alivyotupa ushirikiano na kwa kweli tulipokwenda ofisini Jumatatu alitushauri tuchukue mwili wa marehemu twende tukazike. Kwa vile ametuahidi na kusema tayari amefika mbali katika kulishughulikia suala hili sisi tumeamua kuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuzika,” alisema.

Soma zaidi: Ndugu washikilia msimamo kususia maiti Dar, polisi waeleza upya alivyouawa

Chanzo: mwananchi.co.tz