Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Wazazi wawajibishwe mwanafunzi akipata ujauzito’

2703de246faa2f0be6ac8bd938ae2cf4 ‘Wazazi wawajibishwe mwanafunzi akipata ujauzito’

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“NINAIOMBA jamii ibadilike, iwaache watoto wa kike wasome na kufanikisha ndoto zao mbalimbali. Tatizo ni kwamba wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia wakiwa na umri mdogo kutokana na usimamizi usioridhisha wa wazazi.

“Mtoto akishaharibiwa mwisho wa maisha yake unakuwa mbaya. Anashindwa kujisimamia na hivyo kuwa chanzo cha umaskini.”

Hayo ni maneno ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, anayesisitiza kwamba mwanafunzi akipata ujauzito mzazi anatakiwa kuwajibika kwa kuchukuliwa hatua kwa sababu ameshindwa katika suala la ulinzi na malezi ya mtoto wake.

Mkuu wa mkoa huyo anayasema hayo kutokana na taarifa za kitabu cha mpango mkakati wa mkoa wa Shinyanga katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) kuonesha kwamba katika kipindi cha miaka mitano wanafunzi wapatao168 wamepata ujauzito.

Taarifa katika kitabu hicho zinaonesha kwamba wanafunzi walioacha shule katika kipindi hicho ni 3451, wasichana wakiwa 1628 sawa na asilimia 47.17.

Halmashauri ya wilaya ya Kishapu pekee ina jumla ya wanafunzi 207 walioacha shule katika kipindi hiocho ikiwemo kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Miongoni mwa watoto hao 3451, wanafunzi 1116 waliacha shule kutokana na kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Aidha kitabu hicho kilichozinduliwa hivi karibuni kinaonesha kwamba kesi za ukatili wa kijinsia kwa watoto zilizoripotiwa ni 470 na kesi 159 zipo mahakamani huku kesi 314 zikiwa bado zikichunguzwa.

Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kengese, anasema kuwa suala la mwanafunzi wa darasa la nne wa Shule ya Msingi Ilobi ambalo loliripotiwa na gazeti hili hivi karibu likiwa na kichwa cha habari kisemacho ‘Mimba ya mtoto darasa la nne inazua utata’ amelipata na kwamba linafanyiwa kazi na mamlaka husika.

Katika sakata hilo, binti huyo mjamzito awali alidai kupewa mimba na kaka yake lakini baadaye akabadilisha maneno na kudai aliyempa mimba ni mwalimu wake.

Wakati mama wa mzazi huyo anasema anahisi mwalimu anahusika na mimba ya mwanae, majirani wanatuhumu kaka mtu ambaye wakati makala yale yalipokuwa yakiandikwa alikuwa amekimbia mkoano wa sheria.

Kengese anasema kesi nyingi za wanafunzi kupewa mimba zimekuwa na tatizo la kupatikana kwa ushahidi mzuri kutokana na wazazi kumalizana kimyakimya na wahalifu huku wakimtaka mtoto aliyedhulimiwa kwa kupewa mimba abadilishe maneno ili kuficha au kuharibu ushahidi.

“Inawezekana kweli huyu binti alipewa mimba na ndugu yake… Sasa tumeanza kufuatlia kwa ukaribu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuweza kubaini ukweli. Jamii kila siku inaelimishwa juu ya kumkatili mwanafunzi wa kike masomo yake lakini kuna watu bado hawasikii na mambo yale yale yanajitokeza,” anasema Kengese.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kishapu, Juma Swalala, anasema kuwa suala la mwanafunzi huyo kupewa ujauzito huku yeye akibadilisha msimamo wa awali wamelipata na kulifuatilia.

“Mara nyingi maelezo ya awali anayosema mwanafunzi huwa ndiyo ya kweli. Huyu anaweza kuwa amefundishwa baadaye amtaje mwalimu lakini tumeanza kufuatilia suala hilo kwa ukaribu,” anasema Swalala.

Mwakilishi kutoka taasisi ya UN-Women nchini, Jacob Kayombo anasema kuwa watoto wengi maeneo ya vijijini wanapata mateso na kuishi maisha ya umasikini kwa kuchangiwa na wazazi wao, sio kwamba hawana akili bali hawakutengenezewa mazingira mazuri wakati wa makuzi yao.

Kayombo anasema watoto wa kike wamekuwa wakifanya kazi nzuri na zenye kuonekana kwani walio wengi wakipata bahati ya kusoma wamekuwa wakifika hatua ya maendeleo.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sifuni Msangi, anasema kutokana na kushamiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, mwaka 2017/2018 wizara hiyo ilianza kutekeleza mpangokazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto.

Mwakilishi kutoka ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kitengo cha jinsia, Mwajina Lipinga, anasema matukio ya watoto kupewa mimba na mtu wa karibu ya familia yapo na kwamba sababu kuu ni kukosa malezi na makuzi katika familia husika pamoja na usimamizi wa hovyo wa wazazi.

Lipinga anasema siku hizi kuna kundi kubwa la vijana ambao wamekuwa wakitumia dawa za kuongeza nguvu ambapo hawatumii nguvu hizo kufanya kazi na kujiongezea kipato badala yake wanatumia hizo nguvu kufanya vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike wenye umri mdogo.

“Suala la watoto wa kike kupata mimba katika umri mdogo tumekuwa tukilikemea kwani ndugu wa karibu na familia hata wakipeleka mashtaka kwenye vyombo vya sheria hukosekana ushahidi kutokana na kulindana na mwisho mwanafunzi huyo anakuwa amekosa mwelekeo wa kimaisha,” anasema Lipinga.

Mwakilishi kutoka Shirika la idadi ya watu duniani (UNFPA), Dk Wilfred Ochan anasema kuwa ukatili wa kijinsia ingawa hufanyika kwenye kimwili, huacha madharamengi ya kisaikolojia.

Anasema ndoa za mapema pia zina athari nyingi ikiwa ni pamoja na kuzorotesha hali ya msichana kiuchumi na kimaendeleo.

Dk Ochan anasema wanawake na wasichana wamekuwa wahanga wa aina zote za ukatili wa kijinsia kwa kukosa haki zao za msingi kwani wanapokuwa katika umri mdogo huwa wanashirikishwa zaidi kwenye masuala ya kutunza familia na kukosa fursa ya elimu ikiwemo muda wa kujisomea kama wenzao wanaume.

Chanzo: habarileo.co.tz