Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi waeleza walivyolala na maiti wakiamini mtoto wao amezimia

95116 Mtoto+pic Wazazi waeleza walivyolala na maiti wakiamini mtoto wao amezimia

Mon, 10 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wazazi wa mtoto Meyles Kabuti (3) aliyefariki kwa kudaiwa kupigwa na mwiko kichwa na dada wa kazi kwa kosa la kukataa kula chakula, wameeleza walivyolala na maiti usiku kucha wakiamini mtoto wao hajafa.

Licha ya kupatiwa majibu kutoka kwa daktari kuwa mtoto wao amefariki dunia, wao waliamini amezimia hivyo atazinduka kwani mwili wake ulikuwa wa moto muda wote.

Akizungumza na Mwananchi juzi nyumbani kwake Nkonze jijini Dodoma, mama mzazi wa Meyles, Ashura Kabuti alisema Februari 4 aliondoka asubuhi kwenda kazini na kumuacha mtoto na dada wa kazi.

Ashura ambaye ni mwalimu katika Sekondari ya Nkonze alisema akiwa shuleni saa 3:00 asubuhi alipiga simu kwa dada wa kazi, Agness (waliyemtaja kwa jina moja) ili kumjulia hali mtoto baada ya kuongea naye mtoto alisema anataka kulala.

“Mwanangu anasoma chekechea shule ya Ebeneza ipo tu hapa Nkonze, nilivyopiga simu nikamuuliza mwanangu, baba leo hujaenda shule, akaniambia nataka kulala, nikamwambia sawa, nikahisi pengine alicheza sana hivyo amechoka,” alisema.

Alisema ilipofika saa 7:05 mchana alipokea ujumbe mfupi kutoka kwa Agness akimwambia kuwa mtoto hajaamka tangu alivyolala saa 4:00 asubuhi baada ya kunywa chai.

Pia Soma

Advertisement
Ashura alisema alivyopokea ujumbe huo alihofia akidhani mtoto anaumwa ndiyo maana amelala, jambo ambalo lilimfanya kutoka shuleni hadi nyumbani huku akimpa taarifa hizo mumewe Michael Kabuti.

Umbali wa kutoka shuleni hadi nyumbani kwa Ashura ni sehemu ya kutembea kwa dakika 18, wakati huo alikuwa akiwasiliana na mtu wa bodaboda ili amfuate kwa lengo la kuwahi nyumbani na kumpeleka mtoto hospitali.

Alisema alipofika nyumbani alimkuta mtoto amelala kitandani alipojaribu kumuamsha Meyles hakuamka, hivyo akaamua kumpeleka hospitalini kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Nikaondoka kwenda hospitali wakati nipo njiani nikamuona mume wangu anaelekea nyumbani akitokea kazini kwake, tukaenda naye hospitali ya Aga Khan, madaktari wakaanza kumhudumia mtoto wakaniambia nitoke nje, baada ya muda mume wangu akatoka akasema mtoto amefariki,” alisema Ashura na kuongeza:

“Ukweli hatukuamini taarifa hizo tulihisi madaktari wanatudanganya, tukaamua kurudi nyumbani na mtoto, nilipofika nikamlaza kitandani kuangalia mgongoni nikaona kuna alama za kupigwa ambazo zinaonekana damu imeganda ndani.”

Alisema mumuwe alimuita Agness na kuanza kumhoji alama zilizopo kwenye mgongo wa mtoto ni za nini, ambapo yeye alisema hajui zimesababishwa na kitu gani.

Alisema baada ya kuendelea kumhoji walimwambia Agness kuwa daktari amesema mtoto amekufa, maneno hayo yalimfanya Agness kusema alimpiga kidogo na mwiko mgongoni.

Pia, alisema walimhoji Agness inakuaje mtoto umpige na mwiko mgongoni halafu afariki, swali hilo lilimfanya Agness kueleza yale aliyokuwa anamfanyia mtoto kuwa alimpiga na kiatu kichwani.

Alisema wakati mahojiano hayo yanaendelea tayari ilikuwa imeshafika usiku, hivyo aliamua kulala na mtoto akisubiria azinduke.

Alisema hadi asubuhi ilipofika mtoto huyo hakuzinduka licha ya kuwa mwili wake haukuwa umekakamaa ishara ya kuwa amekufa mwili zaidi ya kulegea.

“Kulivyokucha kuna baba mmoja alikuja baada ya kupata taarifa hizo akasema ni kweli mtoto amefariki, kidogo nikamwamini maana yeye ni mtu mzima japo sikuwa na uhakika sana na kile alichokuwa akikizungumza,” alisema.

Alisema kutokana na maelezo ya huyo baba na ya Agness waliamua kwenda kituo cha polisi wakiwa na Agness na mwili wa mtoto wao ili kutoa taarifa za tukio hilo.

Alisema baada ya taratibu za polisi kufanyika walitakiwa kuhifadhi mwili wa mtoto katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Maisha yao na Agness

Alisema Agness waliiishi naye vizuri takriban miaka miwili kama ndugu yao japo kulikuwa na matukio ambayo alikuwa akiyaona kwa mtoto.

“Kipindi cha nyuma kuna siku nilimuona mwanangu ana alama za kukwaruzwa shingo kama vile kuna kitu kimemchana, nilipomuuliza aliniambia anamshika nyau (paka) mkia na wakati mwingine anakwaruzika akiwa anacheza na mwenzake,” alisema.

Ashura alisema mtoto wake alikuwa anapenda sana wanyama hivyo alichukua uamuzi wa kumfukuza paka akiamini ndiyo chanzo cha mwanaye kuwa hivyo.

Kauli ya baba mzazi

Baba mzazi wa mtoto huyo, Michael Kabuti alisema taarifa ya mtoto huyo kulala bila kuamka alizipata kutoka kwa dada wa kazi na mkewe, akiwa kazini kwake eneo la Majengo Dodoma.

Kabuti alisema baada ya taarifa hizo aliamua kwenda nyumbani na alipofika njiani alikutana na mkewe akielekea hospitalini hivyo wakaongozana.

Alisema majibu waliyopatiwa na daktari hawakuyaamini hivyo kuamua kurudi nyumbani na mtoto wakiamini amezimia hivyo atazinduka.

Alisema walipofika nyumbani walimhoji dada wa kazi kwamba shida ilikuwa ni nini, hali iliyomfanya Agness kueleza alichomfanyia mtoto.

Alisema walikaa na maiti ya mtoto wao usiku kucha wakiamini angezinduka, lakini kulivyokucha waliamua kwenda polisi kuripoti.

Hata hivyo, Kabuti alisema baada ya tukio hilo waliendelea na taratibu nyingine za mazishi ambayo yalifanyika Februari 6. Licha ya dada huyo kueleza alichomfanyia mtoto, hakuna aliyempiga.

Alisema hata sasa wanashangaa kilichosababisha dada wa kazi kufanya tukio hilo, kwani hakuwa na tatizo na mtu yeyote.

Bibi asimulia

Pili Salum ni bibi wa mtoto aliyekufa anasema Februari 4 alipata taarifa ya tukio hilo, hivyo akafika nyumbani hapo kujua zaidi.

Alisema alifika nyumbani hapo usiku na kukuta baadhi ya wanafamilia wakimhoji Agness.

Bibi huyo alisema Agness alisema mtoto alikataa kula akaanza kumpiga akakimbia na kuangukia kwenye kitanda akamfuata akamweka chini na kumkanyaga tumboni karibu mara sita, akachukua kiatu na kumpiga kichwani na mtoto huyo hakuamka.

Alisema mama wa mtoto hakuwa amewahakikishia kuwa mwanaye amefariki bali amezimia, hivyo wakaamua kuondoka.

Pili alisema mama wa mtoto huyo alilala na mwili wa mwanaye hadi asubuhi.

Alisema Februari 5 asubuhi walifika nyumbani hapo kisha kuelekea polisi na taratibu nyingine zilifanyika ikiwamo kuhifadhi mwili mochwari.

Februari 6, walifanya ibada ya kuaga mwili na taarifa zilizosomwa kutoka kwa daktari zilieleza kuwa mtoto huyo amefariki baada ya bandama kupasuka.

Pili aliwataka wazazi tujenga tabia ya kuwakagua watoto kila wanaporudi kutoka kazini hata kama wanawaamini dada wa kazi.

Pia, alisema kutokana na tukio hilo wanaviachia vyombo vya dola vifanye kazi yake na dada huyo wa kazi anashikiliwa Polisi.

Jirani asimulia.

Christina Mdede ni jirani wa familia hiyo, alisema alishangaa kupata taarifa za msiba wa mtoto huyo kwani hakuwa anaumwa.

Alisema Februari 6 walifanya mazishi na wakati wasifu wa mtoto unasomwa waliambiwa alipigwa tumboni na kusababisha bandama kupasuka.

Kuhusu Agness, Christina alisema alikuwa anaishi na watu vizuri na hakuwahi kumuona ana tatizo lolote, ila anashangaa ilikuaje akafanya matukio la aina hiyo.

Alipotafutwa kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, Gilless Muroto kuhusu kushikiliwa kwa dada huyo wa kazi, alikiri na kwamba wanamshikilia kwa uchunguzi zaidi.

Chanzo: mwananchi.co.tz