JESHI la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kupatikana na pembe mbili za ndovu na vipande kadhaa vya pembe hizo vyenye jumla ya thamani ya Sh milioni 89.6.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Fortunatus Muslimu alisema kuwa, tukio la kwanza lilitokea Novemba 11, mwaka huu majira ya saa 1:00 usiku maeneo ya Shule ya Msingi Mtawala, kata ya Mwembesongo, Manispaa ya Morogoro.
Alisema askari wa jeshi hilo kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori walimkamata Muhidin Kidugilike (45) mkazi wa Doma, wilaya ya Mvomero akiwa na vipande viwili vya pembe za ndovu. Alisema askari hao walipapa taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna watu wana pembe za ndovu na kwamba walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na vipande hivyo vikiwa vimewekwa kwenye mfuko wa salfeti.
Alisema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika. Katika tukio jingine, Kamanda Musilimu alisema askari polisi wakiwa doria walimkamata Elitwaza Mbwambo (38) mkulima na mkazi wa kijiji cha Kidodi, wilaya ya Kilosa baada ya kukutwa na pembe mbili za ndovu na vipande vinne vya pembe hizo.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Novemba 19, mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku katika kijiji cha Kifinga, wilaya ya Kilosa. Alisema baada ya kukamatwa na alipopekuliwa mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na pembe mbili za ndovu na vipande vinne vya pembe hizo bila kibali akiwa amezihifadhi katika mfuko wa sandarusi na kubeba mgongoni kama mzingo wa kawaida.
Kamanda Muslimu alisema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo na anafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika na thamani ya nyara zote hizo ni Sh milioni 89.6