Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili mbaroni wizi mitihani darasa la saba

D4d4fd23841ed37f4a2564637c192a59.jpeg Wawili mbaroni wizi mitihani darasa la saba

Wed, 8 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JESHI la Polisi mkoani Mbeya limewakamata watu wawili kwa tuhuma za udanganyifu na wizi wa mitihani ya darasa la saba inayoanza leo nchini.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ulrich Matei alisema jana kuwa, Septemba 4, mwaka huu saa 1:00 usiku maeneo ya Chimala, wilayani Mbarali mkoani humo polisi waliwakamata watuhumiwa wawili (majina yamehifadhiwa) kwa tuhuma za udanganyifu na wizi wa mitihani ya darasa la saba.

Alisema mtuhumiwa mmoja anayedaiwa kuwa kinara wa mpango hao aligundua polisi wanamtafuta na alikamatwa akiwa kwenye mpango wa kutaka kutoroka kwenda Sengerema mkoani Mwanza.

Alisema baada ya kumkamata, kumhoji na kumpekua, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na wizi wa mitihani tangu mwaka 2006 akiwa katika mikoa mbalimbali aliyowahi kufanyakazi akishirikiana na wenzake.

“Mtuhumiwa alikiri kuwa yeye ndiye kinara wa wizi wa mitihani hapa nchini hususani kwa shule binafsi za michepuo wa kiingereza. Ametaja shule 10 zilizopo hapa mkoani Mbeya na nje ya mkoa,” alisema Kamanda Matei.

Juzi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alionya kuhusu wizi wa mitihani hiyo na akawaeleza wasimamizi waache tabia ya udanganyifu na kuvujisha.

Alitoa onyo hilo jana alipokwenda kukagua shule ya mfano ya Iyumbu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz