Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili mbaroni wakituhumiwa kubaka watoto

Thu, 22 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kahama. Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za ubakaji huku mmoja akituhumiwa kuishi kinyumba na mtoto wa miaka 15 na mwingine kwa kumwingilia kimwili mtoto wa miaka mitano.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Simon Haule amemtaja anayeshikiliwa kwa tuhuma za ubakaji kwa kuishi kinyumba na mtoto wa miaka 15 kuwa ni Eresto Jeremia (53) mkazi wa Mwendakulima wilayani Kahama.

“Mtuhumiwa alimlaghai mtoto huyo kuwa angemtafutia kazi za ndani lakini hakutekeleza ahadi hiyo badala yake akaamua kuishi naye kinyumba kama mume na mke,” alisema Kamanda Haule.

Amesema mtuhumiwa mwingine, Simon Patrick (29) mkazi wa Nyahanga mjini Kahama anadaiwa kumbaka mtoto wa miaka mitano baada ya kumvutia chumbani kwake.

“Watuhumiwa wote wawili wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi ukikamilika,” alisema.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumekuja siku moja baada ya juzi mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamlingi Macha kutangaza kiama cha wanaume wakware wanaowanyemelea watoto wadogo na kuwabaka au kuwalaghai kutimiza tamaa zao za mwili.

Akifunguza kikao kazi cha Chama cha Wandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga kilichoandaliwa kwa pamoja na Shirika lisilo la Kiserikali la kutetea na kulinda haki za watoto la Save the Children, mkuu huyo wa wilaya aliapa kula sahani moja na wabakaji na wanaooa watoto wadogo kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa mratibu wa mradi wa kutokomeza ndoa za utotoni na mila potofu kutoka Save the Children, Mary Kyando mkoa wa Shinyanga unaongoza Kitaifa kwa kuwa na asilimia 59 ya ndoa za utotoni. Wastani wa Kitaifa ni asilimia 37.



Chanzo: mwananchi.co.tz