Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili mbaroni kwa mauaji ukumbi wa Disko

Disko Pic Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo akizungumza ofisini kwake

Fri, 14 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limewakamata watu wawili huku likimtafuta mtu mmoja kwa tuhuma za mauji ya Mahadhi Selemani Humbu (20).

Tukio hilo lilitokea katika ukumbi wa disco ujulikanao kama ‘The Don’ uliopo Kata ya Ziwani katika Halmashauri ya Wilaya Mtwara June 30 mwaka huu baada ya kuzuka kwa ugomvi.

Akizungumza ofisini kwake leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Nicodemus Katembo amesema kuwa ugomvi ndiyo uliosababisha kifo cha Humbu mkazi wa Kijiji cha Majengo katika halmashauri hiyo.

Amesema kuwa kijana huyo alifariki njiani kabla ya kufikishwa hospitalini kufuatia jeraha ubavuni upande wa kushoto, lililotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Anayedaiwa kufanya kitendo hicho ni Ally Salum maarufu kama Chepe.

“Inaoneka kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliozuka baina ya marehemu na mtuhumiwa Ally Salum ambapo baada ya tukio hilo alitokroka na hadi sasa jitihada za kumtafuta zinaendeleea ili sheria iweze kufuata mkondo wake,” amesema.

Katika tukio hilo watu wawili walikamatwa kwa mahojiano zaidi ambao ni Aziz Salum Mkumba (32) mkazi wa Kijiji cha Mkubiru pamoja na Shaibu Bakari Mpoyo (33) mlinzi wa ukumbi wa Ziwani kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.

“Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa kifo chake kimesababishwa na kuvuja kwa damu nyingi kutokana na jeraha alilokuwa nalo la kuchomwa na kitu chenye ncha kali,” amesema na kuongeza;

“Upelelezi wa shauri hili unaendela na mara baada ya kukamilika, jalada litawasilishwa Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya hatua zaidi. Natoa wito kwa wote wenye kumbi za starehe kupata vibali vya kupiga disko kutoka katika mamlaka za serikali na jeshi la Polisi.”

Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi linakusudia kufanya msako mkali kwa kumbi zote zinazopiga muziki bila kuwa na vibali na hatua kali zitachukuliwa kwa wamiliki wa kumbi hizo.

Ally Humbu baba wa marehemu alisema kuwa alipata taarifa majira ya saa tisa usiku baada ya tukio hilo.

“Nilipoata taarifa usiku saa tisa kuwa mwanangu amefariki kwa kuchomwa kisu akiwa disko, na kwamba amepelekwa Ligula, nilienda haraka; niliambiwa kuwa amechomwa kwenye mbavu na kukugusa kwenye bandama ambapo ilipelekea damu kutoka nyingi zaidi,” alisema Humbu.

Chanzo: Mwananchi