Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili kortini wakidaiwa kughushi cheti cha kifo, kujipatia Sh102 milioni

Mizani Ya Haki Wawili kortini wakidaiwa kughushi cheti cha kifo, kujipatia Sh102 milioni

Wed, 28 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Mfanyabiashara Samwel Gombo na mwenzake Musa Chiduo wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka matano likiwemo la kughushi cheti cha kifo na wizi wa Sh102 milioni.

Makosa mengine ni kughushi mukhtasari wa kikao cha familia, nguvu ya kisheria pamoja na kuwasilisha nyaraka za uongo katika Mahakama ya Mwanzo Chakwale iliyopo wilayani Gairo, Mkoa wa Morogoro.

Samwel na Musa ambao ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wamesomewa mashtaka yao leo Juni 28, 2023 na Wakili wa serikali, Mosie Kaima mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalila.

Akiwasomea hati ya mashitaka, Wakili Kaima amedai kuwa shitaka la kwanzana linamuhusu Gombo pekee ambapo katika tarehe tofauti kati ya Novemba 13, 2017 na Juni 30, 2018 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam aliiba Sh102 milioni mali ya Stanford Gombo kutoka benki ya NMB.

Hata hivyo, shtaka la pili na la tatu ambalo pia linamhusu mshitakiwa Gombo, inadaiwa tarehe isiyofahamika Novemba 2017 ndani ya Mkoa wa Dar es salaam kwa nia ya kudanganya alighushi cheti cha kifo chenye namba 1003-795-989 kikionesha kimetolewa na wakala wa usajili, ufilisi na udhamini (RITA), wakati ni uongo.

Pia Oktoba10, 2017, Gombo alighushi nguvu ya kisheria ikionesha kuwa ni halali na imetolewa na Stanford Gombo huku akujia sio kweli.

Kwa upande wa shtaka la nne, Wakili Kaima amedai kuwa linawahusu washtakiwa wote wawili ambapo inadaiwa kuwa Januari 17, 2018 katika kijiji cha Kilimani Chakwale kilichopo Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, walighushi muhtasari wa kikao cha familia ukionyesha umeandaliwa na familia ya Stanford Gombo, wakati wakijua sio kweli.

Wakili huyo alidai shitaka la tano ni la Gombo peke yake ambapo Oktoba 31, 2017 katika Mahakama ya Mwanzo Chakwale iliyopo Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, aliwasilisha hati ya nguvu ya kisheria ya uongo ikionesha imetolewa na Stanford Gombo kinyume na kifungu 342 na 338 kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo 2022.

Washitakiwa wote walikana kuhusika na mashitaka hayo.

Wakili Kaima alidai kuwa upelelezi umekamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa hoja za awali (PH).

Kesi hiyo imehairishwa hadi Julai 12, 2023; washtakiwa wamerudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini.

Mahakama ilitoa masharti ya dhamana dhidi ya Gombo ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho na kuwasilisha pesa taslimu Sh51 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Kwa upande wake Mussa, naye alishindwa kutimiza masharaiti ya dhamana ambayo yalikuwa ni wadhamini wawili wenye barua za utambulisho watakao saini bondi ya Sh1 milioni.

Chanzo: Mwananchi