Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili kortini kwa kuzalisha Konyagi, K-Vant bandia, wanadaiwa pia kugushi stempu za ETS za TRA

85159 Pic+konyagi Wawili kortini kwa kuzalisha Konyagi, K-Vant bandia, wanadaiwa pia kugushi stempu za ETS za TRA

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wafanyabiashara wawili wamefikishwa mahakamani kwa makosa 11 ya kuzalisha pombe kali bandia na kugushi stempu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuzibandika katika pombe hizo.

Watuhumiwa hao wanatuhumiwa kukutwa na shehena ya pombe kali bandia aina ya Rivela Gin, Azura Vodka, K-Vant na Konyagi ndani ya nyumba iliyopo Bomang’ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro

Wafanyabiashara hao ambao wameshitakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi likiwamo kosa la kutakatisha fedha ni Godfrend Godson Mlangu (28) mkazi wa Arusha na Crispin Juvenaly Mlangu (21) mkazi wa Hai.

Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Moshi, Jullieth Mawolle na kusomewa mashitaka yao na wakili wa Serikali kutoka Divisheni ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Lilian Kowero.

Akisoma mashitaka hayo, wakili Kowero alidai kuwa Oktoba 29, 2019, washitakiwa pamoja na watu wengine watatu ambao hawajakamatwa, walisuka njama za kuzalisha pombe bandia.

Mbali na kosa hilo, lakini siku hiyo pia wanatuhumiwa kugushi stempu 4,312 kwa lengo la kuonyesha kuwa zilitolewa na TRA, wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Kwa mujibu wa wakili huyo, siku hiyo pia washitakiwa waligushi alama za biashara za kampuni za Tanzania Distilleries Ltd inayozalisha Konyagi na Mega Beverages Co Ltd inayozalisha K-Vant.

Alama za kampuni nyingine wanazotuhumiwa kugushi ni za Blue Nile Distilleries inayozalisha Rivella Gin na Quality Beverages Co Ltd inayozalisha pombe aina ya Azura Vodka.

Pia, wanashtakiwa kutengeneza chupa 192 za pombe bandia aina ya Konyagi, chupa 180 za pombe kali aina ya Rivella, chupa 140 za bombe pandia ya K-Vant na chupa 960 za Azura Vodka.

Mshtakiwa wa kwanza, Godfrend ameshitakiwa kwa kosa la utakatishaji wa fedha akidaiwa kununua gari aina ya Toyota Noah namba T105 DFV kwa kutumia fedha ambazo ni zao la uhalifu.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kama itapata kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) na upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Hakimu Mawolle alisema shitaka la 11 la kutakatisha fedha linalomkabili mshitakiwa wa kwanza halina dhamana, na kwamba kesi itatajwa Novemba 25,2019 kwa ajili ya kupanga masharti ya dhamana baada ya upande wa mashitaka kuwasilisha thamani ya uhujumu wanaodaiwa kuufanya.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao, kunatokana na taarifa za siri alizopelekewa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, na baadaye kuwashirikisha polisi waliozingira nyumba hiyo na kuwakamata.

Chanzo: mwananchi.co.tz