Kufuatia tukio la kuvunjwa kwa ofisi ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) wilayani hapa na kuibiwa kwa bastola mbili na risasi 50 Novemba 30, 2022, leo watu wa wawili wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na makosa manne yanayohusu tukio hilo.
Watu hao wametajwa kuwa ni pamoja na James Alex (48) mkazi wa Vibaoni na Ally Waziri (24), Mkazi wa Bomani aliyekuwa mlinzi wa ofisi hiyo.
Akiwasomea mashtaka hayo leo Ijumaa Januari 6, 2023 katika mahakama ya wilaya Handeni, Mwendesha Mashtaka Seif Makono, mbele ya Hakimu, Veronica Siao amesema, watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ambayo ni pamoja na kuvunja ofisi usiku, wizi, kula njama ya kufanya uhalifu na kushindwa kuzuia uhalifu kufanyika kwa mshtakiwa Ally Waziri, ambaye alikuwa ni mlinzi wa ofisi hizo.
Mwendesha mashitaka Makono ametaja makosa mengine kuwa ni kula njama na uzembe wa kushindwa kuzuia uhalifu kufanyika, ambapo kosa hilo ni kwa mshtakiwa wa pili peke yake.
Ameongeza kuwa baada ya upelelezi kufanyika watuhumiwa hao wawili walikamatwa na kuhojiwa na kufikishwa mahakamani hapo leo Ijumaa.
Amedai kuwa baada ya kuvunja ofisi hizo, watuhumiwa hao waliiba bastola mbili, ikiwamo yenye namba za usajili, CAR NO F. 40326W na risasi 15 na bastola yenye namba za usajili, CAR NO 066206 na risasi 35, zote zikiwa na thamani ya Sh5 milioni mali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa wamefanikiwa kupata dhamana, baada ya kutimiza masharti na shauri hilo la upelelezi limekamilika na litaanza kusikilizwa Januari 20 mwaka huu.