Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili Dar washikiliwa kwa tuhuma za ujambazi, utekaji na uporaji

28491 Mambosasa+pic TanzaniaWeb

Fri, 23 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za ujambazi, utekaji na uporaji wa pikipiki.

Watu hao wamekamatwa kufuatia uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo baada ya kupata taarifa za kutekwa dereva wa bodaboda.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 23, 2018 amesema polisi walipata taarifa kuhusu wahalifu hao na gari wanalolitumia kufanya uhalifu aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T354DPF.

Amesema baada ya taarifa hizo walianza kuwafuatilia ndipo walipolikuta gari hilo Chanika baada ya wahalifu kulitelekeza walipobaini wanafuatiliwa.

Mambosasa ameeleza polisi walilichunguza gari hilo ndipo walipomkuta dereva huyo wa bodadoda Pius Giwes akiwa amefungwa mikono na uso wake kufunikwa.

“Tuliendelea na uchunguzi na hatimaye tumefanikiwa kuwapata watu wawili ambao tunaendelea kuwahoji kutokana na uhalifu huo, ila kwa taarifa tulizonazo wamefanya matukio katika maeneo mbalimbali ya jiji.”

Pia jeshi hilo linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kukamatwa wakiwa na vipande 18 vya meno ya tembo.

Watu hao walikamatwa Novemba 21,2018 eneo la Makangarawe wakiwa na meno hayo wameyaficha kwenye mabegi ya mgongoni.

Katika hatua nyingine jeshi hilo limepiga marufuku watu kuratibu mbio, matembezi ya hisani, maandamano bila kuwa na kibali cha polisi.

Mambosasa amesema hilo limekuwa likisababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara hasa viongozi wakati mwingine wakikwama njiani kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu.



Chanzo: mwananchi.co.tz