Watu wasiojulikana idadi yao wamevunja Kanisa la Anglikana katika mji mdogo wa Magugu wilayani Babati, mkoani Manyara na kuiba vifaa vya kwaya.
Katibu wa Kanisa hilo, Steven Robert amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Februari 3, mwaka huu.
Robert alisema watu hao walivunja moja ya madirisha ya Kanisa hilo na kuingia ndani kisha wakaiba baadhi ya vifaa vya kwaya.
Alitaja vifaa vilivyoibwa kuwa ni kinanda, ‘booster’ na vifaa vingine vya muziki vyenye thamani ya Sh7 milioni.
Alisema wizi huo umetokea katika hilo licha ya kuwa na mlinzi anayelinda mali za kanisa hilo.
“Wimbi la kuvunjwa makanisa na mali kuibwa kwenye eneo hili la Magugu linaendelea kwani makanisa matatu yameshavunjwa,” alisema Robert.
Mmoja wa waumini wa kanisa hilo, John Matle alieleza kusikitishwa na kitendo hicho akitoa wito wa kuwakamata waliohusika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Benjamin Kuzaga alisema hajapata taarifa za tukio hilo la wizi.
“Ndiyo kwanza nimerejea kazini baada ya likizo fupi, ngoja niulize kwa niliowaachia ofisi,” alisema.