Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wauza ‘unga’ wawaweka wanawake mtegoni

Unga Dawa Wauza ‘unga’ wawaweka wanawake mtegoni

Wed, 21 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanawake nchini wametakiwa kuwa makini wanapoanzisha uhusiano wa kimapenzi na raia wa kigeni kwa sababu wengi wao huingizwa kwenye biashara ya dawa za kulevya bila kufahamu.

Tahadhari hiyo ilitolewa jana na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo alipokuwa akieleza mbinu mpya zinazotumiwa na wafanyabiashara wa dawa hizo haramu.

Jumla ya kilo 200.5 za dawa za kulevya aina ya heroin, cocaine kete 138 na metamphetamine gramu 532.1 zimekamatwa katika kipindi cha miezi mitatu huku watuhumiwa wengi wakiwa ni wanawake.

Alisema katika ukamataji uliofanyika kati Machi 25 na Juni 19, imebainika kuwa wafanyabiashara wa dawa hizo wamebuni mbinu mpya ya kuwatumia wapenzi wao kuhifadhi na kusafirisha dawa za kulevya.

Kamishna Lyimo alisema raia kigeni wamekuwa wakianzisha uhusiano wa kimapenzi na wanawake wa kitanzania ambao wote huwatumia kuhifadhi na kusafirisha dawa hizo. Hali hiyo imesababisha kukamatwa kwa wanawake wengi wa kitanzania baada ya kukutwa na dawa za kulevya wanazohifadhi nyumbani kwa niaba ya wapenzi wao.

“Wafanyabishara hawa kila siku wanabuni mbinu mpya hasa raia wa kigeni. Wanakuja nchini inawezekana kwa shughuli nyingine kabisa, ila pia wana hizo biashara, sasa inapokuja jinsi ya kuzifanya wanalazimika kutafuta wanawake wa kitanzania.

Kamishna Jenerali Lyimo alieleza kuwa wanaume hao mara nyingi huwa na mwanamke zaidi ya mmoja ambao wote huwatumia kuhifadhi dawa hizo. “Akishampata hawaishi nyumba moja, hivyo anatumia mwanya huo kuficha mizigo yake kwa yule mwanamke wakati mwingine bila hata kumwambia ni mzigo gani kwa kuwa unafungwa vizuri,” alisema Lyimo.

Alisema kinachoendelea baada ya mzigo kuhifadhiwa, mfanyabiashara huyo kuwaelekeza wateja wake kufuata mzigo nyumbani kwa mpenzi wake au kumuagiza apeleke sehemu wakati mwingine bila kujua amebeba mzigo gani. Kulingana na Kamishna Jenerali Lyimo, mzigo mkubwa uliokamatwa katika operesheni hiyo ulikutwa kwa wanawake na walipohojiwa waliwataja wapenzi wao ambao hata hivyo, waliwakana.

“Niwasihi dada zetu wawe makini wanapoingia kwenye uhusiano hasa na raia wa kigeni, pia usikubali kubeba au kuhifadhi kifurushi usichojua kina nini ndani, mzigo mkubwa tuliokamata tumepata kwa wanawake na wanapowataja wenza wao wanawakana.

“Imetokea mara kadhaa tunapata taarifa sehemu fulani kuna dawa za kulevya, tukienda tunakuta mzigo anao mwanamke anapohojiwa anamtaja mpenzi wake, lakini anakana kwa sababu hajakutwa na ushahidi,” alisema Kamishna Jenerali Lyimo.

Katika ukamataji uliofanyika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha na Kilimanjaro, alisema walikamatwa watuhumiwa 109 wakiwemo raia watatu wa kigeni.

Pia zilikamatwa kilo 1.5 ya bangi iliyozindikwa, magunia 978 ya bangi kavu, magunia 5,465 ya bangi mbichi na ekari 1093 ya mashamba ya bangi, mililita 3,840 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya pethidine.

Alisema pamoja na mbinu hizo zinazoibuka kila kukicha, Lyimo alisema mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha inamaliza tatizo la dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii.

Wakati huo huo, Lyimo alisema Juni 25, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya yatakayofanyika jijini Arusha yakibebwa na kaulimbiu; ‘Tuzingatie utu na kuboresha huduma za kinga na tiba.’

Chanzo: www.tanzaniaweb.live